Fei Toto atoa siri za ndani Yanga, akerwa kutukanwa mama yake

 

Mchezaji wa Yanga aliyekataa kuichezea klabu hiyo Feisal Salum maarufu kama Fei Toto ameendelea kutema nyongo, huku akiwatuhumu baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kuwa walimsingizia kuwa yeye anauza mechi.

Fei Toto amesema kuwa yeye anawapenda mashabiki wa Yanga, ila hawaambiwi ukweli kuhusiana na nini haswa kilichomtoa klabu hiyo ya Yanga aliyoichezea tangu aingie mkataba wa kwanza mnamo mwaka 2018.

“Mashabiki wa Yanga mimi nawapenda ila hawajui kilichonitoa Yanga, nimeondoka Yanga kwa ajili ya manyanyaso,” alisema Fei Toto wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM na kuongeza, ”Mimi niliambiwa na baadhi ya viongozi kuwa ninauza mechi”.

Akiongea kwa huzuni Fei Toto alisema aliambiwa na mtu aliyendani ya kamati ya klabu hiyo kuwa baadhi ya viongozi wanamtuhumu kuwa anauza mechi, ambapo walimueleza kama hataki kucheza mpira arudi kwao Pemba.

“Nilipoambiwa maneno hayo yaliniuma na ilinibidi niwapigie simu wahusika lakini hawakunipokelea simu, ila matusi yakawa mengi na manyanyaso, kunawakati mimi nililia uwanjani lakini watu hawakujua ninalilia nini,” alisema Fei Toto.

Akifananua kuhusu kauli ya kula ugali na sukari, Fei Toto alisema kuwa hiyo ilikuwa ni nyakati za nyuma wakati kabla hajaja mfadhili wa sasa, kwani kunawakati alikuwa anaishi kwa shida bila ya kulipwa mshahara hadi kwa miezi mitatu.

Hata hivyo, amesema tangu ameingia Yanga amekuwa anapitia mengi, ila kwa mshahara huu wa sasa umekuwa na manyanyaso mengi, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa yeye kufikia uamuzi wa kujitoa kwenye klabu hiyo.

“Kuna wakati mama yangu anakuja kuongea na uongozi wanamdhalilisha, mama alikuja Dar es Salaam wakamkalisha Salamander kuanzia asubuhi hadi jioni, kisha wakampeleka Avic Town, haitoshi bado wanamtukana, wanamtolea maneneo mabovu na kejeli,” alisema Fei Toto.

Fei Toto aliyeonyesha kuchukizwa kutukaniwa mama yake amesema, “Mama yangu ndio msimamizi wanngu halafu anajitokeza mtu kapewa simu ya macho matatu anawaaminisha wananchi mimi ni mbaya, anamuita mama yangu andazi!?”.

Chapisha Maoni

0 Maoni