Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Maharage
Chande, amesema wanalazimika kukata umeme inaponyesha mvua kubwa ili kuepusha
madhara kutokana na waya za umeme wanazotumia kutokuwa na (insulator) ganda la nje
la plastiki la kuzuia maji ya mvua yasisababishe hitilafu.
Bw. Chande amebainisha hayo jana usiku Dar es Salaam wakati
akijibu maswali ya wahariri wa vyombo vya habari katika majadiliano
yaliyofanyika kujadili sekta hiyo ya umeme na kuelezea mafanikio na mipango ya
shirika la Tanesco.
Mkurugenzi huyo amesema kwamba sio kweli kama transfoma zao
zinaogopa mvua ama radi, bali ukweli ni kwamba waya wanazotumia hazina maganda
ya kuzilinda hivyo mvua kubwa inaponyesha inaweza kusababisha hitilafu ya umeme.
“Waya tunazotumia kwa sasa hazina ganda la nje la (insulator),
sasa mvua ikinyesha kubwa maji yanasababisha muunganiko wa waya na kupelekea
kutokea shoti ya umeme na kuathiri miundomninu,” alisema Bw. Chande na kuongeza
“Waya zenye ganda ni ghali mno”.
Ukusanyaji madeni ya
umeme
Akiongelea suala la ukusanyaji wa madeni ya umeme kwa wateja
wao wanaodaiwa, Bw. Chande amesema Tanesco imeshatangaza tenda ya kuwapata wataalam
wa kudai madeni na tayari mshindi ameshapatikana.
“Tumetangaza tenda ya kuwapata wababe wa kudai madeni na
tayari mshindi amepatikana, hivi karibuni ataanza kazi mtasikia heka heka, na
sisi Tanesco tupo tayari kwa yatakayotokana na heka heka hizo,” alisema Bw.
Chande.
Umeme wa Jua
Kuhusu matumizi ya umeme wa jua, Bw. Chande amesema jumatato
ya wiki ijayo Tanesco wanatarajia kutia saini mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa
jua, ambao ni mkubwa kuwahi kufanyika katika nchi za Afrika Mashariki.
“Jumatatu ya wiki ijayo Tanesco tutatia saini mradi wa umeme
wa jua wa Megawati 50, nadhani huu utakuwa ni moja ya mradi mkubwa wa umeme wa
jua kuwahi kufanyika kwenye nchi za Afrika Mashariki,” alisema Chande huku
akionyesha hisia za kujivunia mradi huo mkubwa.
Amesema mradi huo wa umeme wa jua utafanyika huko Kishapu, Shinyanga
ambapo umeme wake utaingizwa kwenye gridi ya taifa ifikapo Julai 2024. Kwa sasa
Tanesco inazalisha Megawati 5 tu za umeme wa jua zinazotumika katika mkoa wa
Kigoma.
Matumizi ya Teknolojia
Kuhusu Tanesco katika kuchangamkia matumizi ya teknolojia
Bw. Chande amesema wamekuwa wakishughulikia suala la kuwa na mita janja (smart
meter) walizopata awali zilikuwa ghali lakini kwa sasa wamepata mita janja ambazo
ni nafuu.
“Tumekuwa tukipanga kuanza kutambulisha mita janja, lakini
kwanza tulipata mita ambazo ni ghali sana, ila sasa tumepata mita janja nafuu
hata hivyo mita hizo zinahitaji pia kuwa na mfumo wake wa kuwasiliana na mita
ambao nao unagharama zake,” alisema Bw. Chande.
Pamoja na mambo mengine, Bw. Chande amesema kwamba Tanesco inafikiria
kuanza kutumia magari yanayotumia nishati ya umeme, ili kupunguza gharama za matumizi
ya magari wanayotumia sasa ambayo yanatumia mafuta ya dizeli.
0 Maoni