Mchungaji mtata Odero wanajuana na Mackenzie


Mhubiri mwenye mahubiri yenye utata Ezekiel Odero pamoja na mkuu wa dhehebu tata la Kilifi Paul Mackenzie ni watu wanaojuana, Mahakama ya Shanzu nchini Kenya imeelezwa hii leo.

Wapelelezi wamesema wamebaini uhusiano baina ya Odero wa kanisa la New Life lililopo Mavueni na Mackenzie ambaye anadaiwa kuwashawishi waumini wake kufa njaa ili wakutane na Mungu.

Mwendesha mashtaka wa umma ameiambia Mahakama kwamba kunaushahidi wa uhakika baadhi ya watu waliokufa kwenye kanisa la Odero walizikwa kwenye eneo la Mchungaji Mackenzie la Shakahola.

Wapelelezi wamesema wamefuatilia miamala ya fedha ya shilingi milioni 3 za Kenya baina ya wachungaji hao Odero na Mackenzie kwa ajili ya kununua kituo cha televisheni.

Odero amekiri kununua kituo cha TV kutoka kwa Mchungaji Mackenzie, lakini biashara hiyo haipaswi kuhusishwa na vifo vya waumini zaidi ya 100 huko Shakahola.

Odero, ambaye alilalakatika kituo cha polisi cha Shanzu aliwakilishwa Mahakamani na mwanasheri wake Jared Magolo.

Chapisha Maoni

0 Maoni