Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ametoa wito kwa nchi Wanachama za Ukanda wa Maziwa Makuu kuwapa wanawake nafasi yenye ushawishi katika maamuzi na mazungumzo ya amani, akisisitiza kuwa maazimio ya kuwashirikisha yaambatane na mipango inayotekelezeka na kupimika.
Makamu wa Rais ametoa wito huo, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufungua Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Wabunge Wanawake wa Nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu (FP- ICGLR), unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Amesema wanawake ni viongozi, wapatanishi na wajenzi wa amani ambao mchango wao unapaswa kupewa nafasi katika kuzuia na kutatua migogoro. Ametoa rai ya kuondolewa kwa mila kandamizi, ubaguzi na vikwazo vya kiuchumi vinavyowanyima fursa hizo, huku akihimiza uwekezaji katika elimu, ujuzi na uchumi wa wanawake na vijana ili kujenga msingi imara wa usalama na maendeleo.
Makamu wa Rais, amesisitiza kuwa utekelezaji wa Azimio Namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uonekane katika fursa halisi za maamuzi, elimu, ardhi, mitaji, teknolojia na ajira zenye staha.
Kwa upande wa Tanzania, Makamu wa Rais amesema Serikali imedhamiria na imejizatiti kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika masuala ya amani, usalama na uongozi. Kwa miongo kadhaa, Tanzania imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki katika juhudi za kuimarisha amani na usalama, kikanda na kimataifa. Mfano wa dhamira ya Tanzania katika kukuza ushiriki na nafasi ya wanawake katika uongozi ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kupanua fursa na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa. Kupitia mipango mbalimbali ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, inayoendelea kuwaunganisha wanawake wajasiriamali, hususan wanaomiliki biashara ndogo, za kati na kubwa na fursa za masoko, mitaji na mikopo yenye masharti nafuu. Tanzania inaendelea kutekeleza dhamira na ahadi zake za kitaifa, kikanda na kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, amani na usalama.
Kwa upande wake Rais wa Jukwaa hilo ambaye pia ni Spika wa Bunge la Angola, Adão de Almeida, amesema amani ya kudumu haiwezi kupatikana bila wanawake kushiriki kikamilifu katika mazungumzo, upatanishi na maamuzi ya kisera. Amesema migogoro ya kivita, watu kulazimika kuyahama makazi yao, umaskini na unyonyaji haramu wa rasilimali vinaendelea kuumiza ukanda huo, huku wanawake na watoto wakibeba mzigo mkubwa.
De Almeida ameyataka mabunge ya nchi 12 wanachama kutumia mamlaka yao ya kutunga sheria, kusimamia serikali na kupitisha bajeti kuimarisha nafasi ya wanawake katika uongozi, uchumi na ujenzi wa amani.
Awali, Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, ametoa wito kwa wabunge kuhakikisha sauti, mahitaji na changamoto za wanawake na wasichana zinaonekana katika sheria, sera na bajeti. Amesema Tanzania inaendelea kuimarisha usawa wa kijinsia, huku wanawake wakiwa zaidi ya asilimia 39 ya wabunge na wakiongoza kamati saba za kudumu za Bunge.
Zungu ametaja Mpango Kazi wa Kitaifa wa utekelezaji wa Azimio Namba 1325 kuwa sehemu ya hatua za kuongeza ushiriki wa wanawake katika amani na usalama. Ameeleza matumaini kuwa mkutano huo utatoa tamko litakalofungua nafasi zaidi kwa wanawake kuongoza juhudi za kuzuia migogoro na kujenga amani ya kudumu katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Mkutano huo wa Novemba 2 hadi 5 unaendeleza nafasi ya Tanzania katika historia ya ushirikiano wa Kikanda, ambako Azimio la Dar es Salaam la mwaka 2004 liliweka msingi wa kuundwa kwa ICGLR. Mkutano huo unalenga kuandaa tamko kuhusu wanawake katika ajenda ya amani na mpango wa utekelezaji unaoyapa mabunge jukumu la kusimamia masuala ya ulinzi na usalama.
Mkutano huo unahudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Judith Suminwa Tuluka; Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Bw. Huang Xia, maspika na naibu maspika kutoka nchi za Maziwa Makuu; Spika Mstaafu Mhe. Anna Makonda, Mhe. Balozi Gertrude Mongella, Rais wa kwanza wa Bunge la Afrika (Pan-African Parliament), wabunge na mawaziri; wajumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika; viongozi wa ICGLR na Jukwaa la Mabunge; mabalozi, washirika wa maendeleo na asasi za kiraia. Mkutano huo unaongozwa na Kauli Mbiu “ Ukanda wa Maziwa Makuu Wenye Amani na Maendeleo” (“For a Peaceful and Developed Great Lakes Region”).


0 Maoni