RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kutatua migogoro ya kazi kwa usawa, kwa kuzingatia sheria na kulinda haki za wafanyakazi na waajiri.
Rais Samia amesema hayo leo Novemba 2, 206 wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Amesisitiza kuwa maamuzi kuhusu migogoro ya kazi yanapaswa kuzingatia makosa yaliyothibitishwa bila kujali nafasi au utambulisho wa mtu, ili kulinda haki za wafanyakazi na waajiri, hususan katika kipindi hiki ambacho shughuli za sekta binafsi nchini zinaendelea kupanuka.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu ukiukwaji wa haki hizo, misingi ya utawala bora na utendaji wa taasisi za umma.
Aidha, ameitaka Tume hiyo kulinda maslahi ya nchi kwa kufuatilia nafasi ya Tanzania katika masuala ya utawala bora kimataifa na kutoa ufafanuzi kwa wakati.
Rais Samia pia amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora kusimamia matumizi ya fedha, utekelezaji wa miradi ya Serikali na utatuzi wa kero za wananchi wa mkoa huo.
Walioapishwa ni Angeline Lubala Mabula kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora; Dunford George Mpelumbe kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; na Omar Ali Omar Bhai kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Wengine ni Jaji Mstaafu Wilfred Peter Dyansobera, aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, pamoja na makamishna sita wa Tume hiyo.


0 Maoni