Waandishi wa habari za michezo kimataifa wapewa ubalozi wa hiari wa utalii Tanzania

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb),  Oktoba 9, 2026, amekutana na waandishi nguli wa habari za michezo na burudani kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuwakabidhi vyeti vya utambuzi wa kuwa Mabalozi wa Hiari wa Utalii Tanzania (Goodwill Ambassadors) katika hafla iliyofanyika Hoteli ya The Mora, Zanzibar.

Waandishi hao wamepatiwa vyeti hivyo kutokana na mchango wao katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia kampeni ya “Destination Tanzania” wakati wa Kombe la Dunia, pamoja na ziara yao ya kutembelea vivutio vya utalii nchini iliyoanza Oktoba 2 na inatarajiwa kukamilika Oktoba 11, 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kijaji amewapongeza waandishi hao kwa kujitoa kwao kuitangaza Tanzania na kuwataka kuendelea kuwa mabalozi wa vivutio vya utalii nchini kwa kuitangaza Tanzania katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

“Uzuri mliouona ni kama asilimia moja tu ya uzuri wa Tanzania. Hivyo, mnahitaji kuja tena na tena ili kujionea mengi zaidi,” amesema Dkt. Kijaji.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia utalii na michezo, sambamba na maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza wa mashindano hayo pamoja na Kenya na Uganda.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Utalii na Mambokale Zanzibar, Juma Thabit Kaponda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, waandishi hao ambao baadhi wanaondoka Oktoba 10, 2026 na wengine watahudhuria mechi ya “dabi” ya Simba na Yanga wameeleza kustaajabishwa na uzuri wa Tanzania na watu wake na kuahidi kuendelea kuitangaza Tanzania.






 

Chapisha Maoni

0 Maoni