Vijana Afrika wakutana kunolewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amesema vijana barani Afrika wana mchango katika kutafuta suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika mataifa yao.

Dkt. Muyungi amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya Vijana wa Afrika kuhusu Majadiliano ya Mabadiliko ya Tabianchi yanayofanyika jijini Dar es Salaam yanayoshirikisha vijana kutoka takriban nchi 20.

Alisema ni wakati muafaka sasa kwa vijana kujengewa uelewa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi yanalikabili bara hilo na athari zake hivyo kwa umoja wao kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhu.

Kutokana na umuhimu huo, Dkt. Muyungi alieleza kuwa Tanzania imeazimia kuwaendeleza vijana hatua ambayo inakuja kutokana na maazimio ya viongozi wakuu wa za Afrika waliokutana jijini Addis Ababa, Ethiopia mwanzoni mwaka 2026.

Alisema katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwashawishi viongozi kuifanya nchi hiyo kuwa kituo cha kutoa mafunzo ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

“Kwetu sisi kama Tanzania ni heshima kuwa tumepata kutokana na maono ya Rais wetu ambaye amenejenga misingi ya diplomasia kimataifa na hapa tunashuhudia vijana wamefurahi kupatiwa mafunzo haya, tuna wakufunzi kutoka Tunisia, Afrika Kusini, Gambia na Algeria, nasi tunaahidi tutayaendesha kwa weledi mkubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo kwa vijana pia ni mojawapo ya maandalizi kuelekea Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaotarajiwa kufanyika Antalya nchini Uturuki kuanzia November 9 hadi 20, 2026.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amewataka vijana barani Afrika kushiriki kikamilifu katika majadiliano na maamuzi kuhusu mabadiliko ya tabianchi ili kulinda mustakabali wa bara hili.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanawakutanisha vijana 60 kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Tanzania, Ghana, Madagascar, Eswatini, Tunisia, Afrika, Kusini Kenya, Malawi, Gambia, Zambia, Benin, Nigeria, Uganda na Ethiopia.




Chapisha Maoni

0 Maoni