Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Prof. Efatha Kaaya amewataka watumishi wa Taasisi hiyo kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuzingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na zenye viwango vinavyostahili.
Prof. Kaaya alitoa wito huo jana wakati akizungumza na watumishi wapya na waliohamia katika taasisi hiyo wanaoshiriki mafunzo elekezi ya siku tano yanayofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, uliopo ORCI jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo wa bodi alisisitiza umuhimu wa watumishi hao kufahamu na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ili kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na ufanisi.
"Ni muhimu kwenu kuelewa Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma ili kuhakikisha mafunzo haya yatakayotusaidia kuongeza tija na utendaji wa kazi wa Taasisi yetu," alisema Prof. Kaaya.
"Mafunzo haya ni muhimu katika kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi. Hivyo, nawasihi myazingatie na kuyatumia kwa vitendo katika kazi zenu za kila siku ili kuongeza tija, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora zinazokidhi mahitaji yao," alisema Prof. Kaaya.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Mwenyekiti huyo wa Bodi Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watumishi wapya na waliohamia kuhusu majukumu yao, maadili ya utumishi wa umma na namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Dkt. Msemo alisisitiza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao badala ya kujikita katika malalamiko yasiyochangia upatikanaji wa suluhisho.
Kwa upande wake Mkufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, Hosea George akiwasilisha mada kuhusu Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma aliwasisitiza watumishi hao kuzingatia misingi ya maadili na uwajibikaji katika utendaji wao wa kazi, ikiwemo utii kwa Serikali, bidii na kujituma kazini, utoaji wa huduma bila upendeleo, uadilifu, uwajibikaji kwa umma, kuheshimu sheria na kanuni, pamoja na matumizi sahihi ya taarifa.
"Zingatieni maadili ya utumishi wa umma ambayo ni msingi muhimu wa kujenga imani ya wananchi kwa Taasisi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haki, uwazi na ufanisi. Kila mtumishi ana wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa weledi, kuheshimu haki za wananchi na kutunza siri za Taasisi ili kuimarisha uwajibikaji na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa," alisema George.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za ORCI za kuimarisha uwezo wa watumishi wake, kuongeza tija na ufanisi wa Taasisi pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa na wananchi kwa ujumla.

0 Maoni