Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu amechaguliwa na Baraza la Uongozi la Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja huo.
Uchaguzi huo umefanyika wakati wa Mkutano wa Baraza la Uongozi la IPU uliofanyika katika moja ya ukumbi kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), leo Oktoba 6, 2026.
Mheshimiwa Spika amependekezwa na Spika wa Bunge la Wawakilishi la Uingereza (House of Commons) Sir Lindsay Hoyle na kuungwa mkono na Spika kutoka Falme za Kiarabu na Bunge la Uganda.
Akitoa hoja ya kumpendekeza Mheshimiwa Zungu, Sir Lindsay Hoyle amesema anayo heshima kupendekeza jina la Spika wa Bunge la Tanzania kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja huo.
"Ninayo heshima kumpendekeza Spika wa Tanzania kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), naweza kusema urafiki wa muda mrefu, urafiki wenye mizizi, ndiyo maana kwa heshima kubwa nampendekeza Spika wa Tanzania," amesema Spika Sir. Lindsay.

0 Maoni