Muungano umetajwa kuwa ni msingi muhimu wa Taifa na umeendelea kudumisha umoja, mshikamano, amani na ushirikiano kati ya wananchi wa pande mbili za Muungano.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dkt. Islam Seif Salum wakati akifungua mafunzo maalumu kwa watumishi wa Idara ya Muungano mjini Morogoro leo Oktoba 02, 2026 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Dkt Islam amewataka watumishi hao kuhakikisha kuwa masuala ya Muungano yanasimamiwa kwa weledi, uadilifu na ufanisi hatua itakayochangia katika kuimarisha Muungano.
“Muungano wetu ni wa kipekee barani Afrika na duniani kwa ujumla na hauwezi kuyumba ulikuwepo tutambue tu Muungano ulikuwepo tangu zamani na baadae kurasimishwa rasmi na waasisi wa wake,” alisema.
Pia, Dkt. Islam alieleza kupitia ushirikiano wa Serikali zote mbili zimeendelea kutatua Hoja za Muungano hivyo kupitia mafunzo hayo watumishi watakuwa na wasaa wa kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa majukumu.
Aliongeza kuwa Mwongozo wa Vikao vya kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara, Idara na Taasisi zisizo za Muungano za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali za Mapinduzi ya Zanzibar umeziwezesha kukutana mara kwa mara kwa kupitia vikao na ziara na hivyo kubadilishana uzoefu, sheria, Sera, wataalamu na utaalamu pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoweza kujitokeza katika Muungano.
Hivyo, alisema ni mafunzo hayo yatakuwa ni chachu ya kuongeza uwezo na maarifa ya kusimamia miongozo hiyo kwa weledi ili kuchochea kuimarika na kudumishwa kwa Muungano.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Muungano Ofisi ya Makamun wa Rais Dkt. Juma Mohamed Salum alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo maafisa wa Idara ya Muungano kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Zanzibar katika kutekeleza Mpango wa Elimu wa Elimu kwa Umma kuhusu Muungano.
Aliongeza kuwa kupitia elimu hiyo wananchi watapata uelewa wa masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano ambayo yanatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali zote mbili.
Aidha, Dkt. Juma alisema kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania ni vijana waliozaliwa baada ya Muungano kuungabno hivyo kupitia elimu hii watapata uelewa wa Muungano.

0 Maoni