Serikali kuimarisha vituo vya Tehama vya jamii Zanzibar

 

Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Dkt. Mohammed Ali Suleiman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuboresha vituo vya TEHAMA vya Jamii ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa na kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata ujuzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), utakaowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Dkt. Mohammed ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea vituo vya TEHAMA vya Jamii vilivyopo Kiembe Samaki, Bwefum, Fumba, Mwera, Mkokotoni, Tunguu na Kitogani, ambapo alipata fursa ya kukagua hali ya vituo hivyo, kujionea huduma zinazotolewa pamoja na kusikiliza maoni na changamoto zinazowakabili walimu na wanafunzi.

Amesema Serikali itaendelea kuviimarisha vituo hivyo kwa kuvipatia mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia, ili viwe vituo muhimu vya kuwajengea vijana ujuzi wa TEHAMA unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwawezesha kujiajiri kupitia fursa mbalimbali zinazopatikana katika uchumi wa kidijitali.

Katika ziara hiyo, walimu wa vituo vya TEHAMA vya Jamii, Ndg. Fahmi Rajab Abdallah na Ndg. Fauzia Shukurani Haji, walimweleza Waziri kuwa, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali za kuanzisha vituo hivyo, bado wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitendea kazi pamoja na fursa za kujiendeleza kitaaluma.

Walimu hao waliomba Serikali kuwawezesha kupata mafunzo na fursa za kuongeza ujuzi, sambamba na upatikanaji wa vifaa vya kisasa, ili kuboresha ufundishaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Naye mmoja wa wanafunzi anayenufaika na mafunzo katika Kituo cha TEHAMA cha Jamii Tunguu, Ndg. Fatma Seif Khamis, amesema elimu ya TEHAMA anayoipata imemsaidia kujenga ujuzi wa vitendo unaomwezesha kubuni fursa za kujiajiri na kuongeza kipato.

Aidha, amewahamasisha vijana wengine kutumia fursa zinazotolewa katika vituo hivyo ili kujenga uwezo wao katika teknolojia na kujiandaa kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa inayozidi kutegemea teknolojia na huduma za kidijitali.

Chapisha Maoni

0 Maoni