WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma kwa namna ambavyo wamekuwa wakihamasisha jamii juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mhe. Masauni ameyasema hayo wakati ziara yake ya siku nne Mkoani Kigoma Oktoba 16, 2026 alipotembelea na kukagua Kiwanda cha Mkaa Mbadala kilichopo Wilaya ya Kakonko.
Aidha ametoa wito kwa uongozi wa Wilaya hiyo kuendelea kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji holela wa misitu na uchomaji moto.
Amesema wilaya hiyo ina utajiri mkubwa wa misitu ambayo wakiitumia vizuri jamii itanufaika na Biashara ya Kaboni ambayo baadhi ya Halmashauri nchini tayari zimeanza kunufaika.
“Ukataji wa miti na kutumia kuni kupikia kuna athari kubwa kuanzia kwa mtumiaji kwa kuwa moshi anavuta una madhara yake, miti anayokata inaharibu ardhi na kusababisha athari kubwa zaidi,” amesema Mhe. Masauni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Mhe. Kanali Evance Mallasa amesema Wilaya imeendelea kuimarisha juhudi za utunzaji wa mazingira kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi wa misitu na matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kupunguza ukataji holela wa miti na uchomaji moto.
Katika hatua nyingine, Wilaya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanikiwa kujenga kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala kinatarajiwa kuzalisha wastani wa tani 730 za mkaa kwa mwaka na kuwafikia takribani wananchi 30,000 kila mwaka, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa mkaa wa kuni na kusaidia uhifadhi wa misitu.


0 Maoni