DKT. MWIGULU: Rais Samia ni nyota wa mchezo ukuaji sekta ya madini

WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko na ukuaji wa sekta ya madini nchini.

Amesema kwa maelekezo yake, Serikali imefanya mabadiliko makubwa ya sera ambayo yamewezesha wachimbaji na wachenjuaji wazawa wa madini kukua kiuchumi kwa kuwezeshwa kupata mitaji.

"Tumeona mchango mkubwa wa wachimbaji wazawa kwenye uchumi wa nchi yetu, tunathamini mchango wa wachimbaji wadogo pamoja na wawekezaji wengine ambao wamechangia kukuza uchumi wa nchi yetu," amesema.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokutana na kampuni za uwekezaji katika sekta ya dhahabu za Gold World Council, Stone X na kampuni ya kizawa ya Geita Gold Refinery (GGR) inayomilikiwa na mwekezaji mzawa Mama Sarah Masasi.

Amesema dhahabu imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kupitia DIRA 2050, Serikali imelenga kubadilisha uchumi na maisha ya Watanzania.

"Serikali imeendelea kufanya mabadiliko katika sekta hii na kufanya maboresho ya kisera  ili kukidhi mahitaji ya wachimbaji wadogo na wachenjuaji wa madini jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kupitia sekta hii. Tunatamani kuiona sekta hiyo ikiendelea kukua," amesema.

Pia, Waziri Mkuu amesifu ushirikiano wa kiuwekezaji uliopo baina ya wachimbaji na wachenjuaji wa dhahabu nchini ambao umeendelea kuongeza ukuaji wa sekta hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema sekta ya madini imeendelea kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi na sasa inachangia asilimia 10 katika pato la Taifa.

"Dhahabu imekuwa bidhaa adimu katika soko la fedha la kimataifa na inachangia zaidi ya asilimi 53 ya pato la fedha za kigeni na imekuwa bidhaa imara katika kukuza uchumi wetu, Tanzania tunazalisha zaidi ya tani 65 za dhahabu na mchango wa wachimbaji wadogo ni karibu aslimia 40," alisema.

Alisema kwamba Serikali sasa inatekeleza Sera ya Uchimbaji inayosema "Madini kwa kesho iliyobora" yenye lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana, na sasa Serikali inafuta vibali ambavyo havijaendelezwa na kuwapatia wachimbaji wadogo.

Naye, Mmiliki wa Kampuni ya Uchenjuaji ya GGR, Mama Sarah Masasi aliishukuru Serikali kwa kutoa fursa kwa wachimbaji wazawa kushirikiana na wawekezaji kutoka nje, jambo ambalo limechangia kuongeza mitaji na uwekezaji katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo wa Kampuni ya Stone X, Bw. Jonathan Kay alisema Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanya kazi ya kuipandisha thamani dhahabu ya Tanzania na kwa kushirikiana na kampuni kama GGR wamefanikiwa kukusanya kiwango kikubwa cha dhahabu  kupitia Benki Kuu ya Tanzania na Benki Kuu ya Uingereza.



Chapisha Maoni

0 Maoni