Wakuu wa Taasisi za Muungano Watakiwa Kuongeza Ushirikiano na Kuboresha Huduma kwa Wananchi

Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi amewataka wakuu wa taasisi za Muungano kuongeza ushirikiano katika utendaji ili kuboresha huduma kwa wananchi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

 Ndejembi alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua kikaokazi cha wakuu wa taasisi za Muungano kilicholenga kuongeza ufanisi na ushirikiano wa kiutendaji, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa watendaji kuelewa maana, muundo na majukumu ya taasisi hizo ili kuondoa changamoto zinazoweza kuzorotesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi.

Alibainisha kuwa baadhi ya viongozi hawana uelewa wa kutosha kuhusu Muungano na muundo wake, jambo linalofanya Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, huku akiwataka watendaji kutambua kuwa taasisi za Muungano zinahudumia pande zote mbili za nchi na si kujikita upande mmoja pekee.

Akisisitiza kuhusu mshikamano, alisema kuwa watendaji wanajenga nyumba moja katika utoaji wa huduma na hakuna sababu ya kunyang’anyana fursa kwa kuwa lengo kuu ni kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndiyo wanufaika wakuu.

Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni alisema serikali imejipanga kuongeza elimu ya Muungano kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana na wanafunzi, na kueleza kuwa kikao hicho ni sehemu ya Mpango wa Elimu ya Umma kuhusu Muungano unaolenga kuwafikia viongozi wa serikali na taasisi zake.

Aliongeza kuwa mkutano huo umewakutanisha viongozi wa taasisi za Muungano zipatazo 39 ili wajadili na kubadilishana mawazo kuhusu utekelezaji wa mikakati ya kazi.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Said Mohamed alisema taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake pande zote mbili na imejipanga kuongeza ufanisi ikiwemo kutoa huduma kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Jabir Makame alieleza kuwa mamlaka hiyo ni ya Muungano yenye jukumu la kuratibu masuala ya usafiri wa anga katika pande zote mbili na inashirikiana vizuri na Zanzibar. Jumla ya watendaji wa taasisi 39 za Muungano walikusanyika Unguja, Zanzibar kwa ajili ya kikaokazi hicho cha kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji.

Chapisha Maoni

0 Maoni