Na Mwandishi Maalumu - Dar es Salaam
Ujumbe wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) umefanya ziara katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuangalia huduma, miundombinu pamoja na teknolojia mbalimbali zinazotumika katika Taasisi hiyo kuelekea michuano ya AFCON 2027.
Hatua hiyo iliyofanywa na CAF ni sehemu ya kuhakikisha kuwa huduma bora za afya, ikiwemo miundombinu safi na salama vinapatikana kwa viwango vinavyohitajika wakati wa michuano ya AFCON itakayofanyika nchini mwaka 2027.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Dkt. Peter Kisenge alisema viongozi hao wameweza kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuridhishwa na huduma zetu.
“Kutokana na miundombinu ya kisasa iliyopo JKCI tutaweza kuwahudumia wachezaji watakaopata matatizo hata wakiwa uwanjani ama katika hotel watakazofikia kwa kutumia kifaa maalumu kijulikanacho kama DOZEE kuwekwa chini ya kitanda alicholala mchezaji aliyepata matatizo”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Meneja wa Tiba kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Dkt. Boubakary Sidiki alisema ameridhishwa na maandalizi aliyoyaona JKCI na kueleza kuwa huduma zinazotolewa zinaendana na viwango vya kimataifa.
“Dar es Salaam ipo tayari kwa michuano hii ya AFCON, nimetembelea JKCI nimeona vitu viko kitaalamu kama ambavyo ilivyo Ulaya, naamini wakati wa michuano ya AFCON hatutapata changamoto za huduma za afya kwasababu ya uwepo wa JKCI na hospitali nyingine zilizopo”, alisema Dkt. Sidiki.
Maandalizi hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania katika kutoa huduma za afya kwa washiriki wa AFCON 2027 huku matumizi ya teknolojia za kisasa yakilenga kuwezesha ufuatiliaji wa karibu wa hali za kiafya za wachezaji na washiriki wengine wakati wa michuano hiyo.


0 Maoni