Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Septemba 1, 2026, amehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Zambia, Hakainde Hichilema, zilizofanyika jijini Lusaka, Zambia.
Rais Hichilema amechaguliwa kuiongoza Zambia kwa muhula wa pili, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 13, 2026 nchini humo.
Tanzania na Zambia zimeendeleza ushirikiano wa kindugu na kihistoria, ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, na Hayati Dkt. Kenneth Kaunda wa Zambia. Ushirikiano huo umeendelea kuimarika katika sekta za uchumi, nishati, miundombinu, biashara na uwekezaji, ukichagizwa na miradi ya pamoja inayounganisha maslahi ya nchi hizo na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa.
Miradi hiyo inahusisha ufufuaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ujenzi wa bomba jipya la mafuta la TAZAMA, pamoja na maunganisho ya gridi za umeme kati ya Zambia, Tanzania na Kenya.
Katika muhula wa kwanza wa Rais Hichilema, thamani ya biashara kati ya Tanzania na Zambia iliongezeka kutoka Sh bilioni 320.978 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 820.359 mwaka 2024.
Zambia, ambayo ni mtumiaji wa pili kwa ukubwa wa Bandari ya Dar es Salaam, imewekeza katika miradi 29 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 86.34, iliyozalisha ajira 1,204. Wakati huo huo, Watanzania wanamiliki hisa katika kampuni kubwa na za kati zipatazo 965 nchini Zambia.



0 Maoni