Rais Dkt. Mwinyi azindua kamati ya pamoja ya majadiliano CCM na ACT Wazalendo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuundwa kwa Kamati ya Pamoja ya Majadiliano yenye wajumbe kutoka CCM na ACT Wazalendo ni hatua muhimu katika kuendeleza mchakato wa maridhiano na kuimarisha amani, umoja na utulivu wa kisiasa Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 14 Septemba 2026, Ikulu Zanzibar, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kamati hiyo, akiwataka wajumbe kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, kuheshimiana na kuweka mbele maslahi mapana ya Zanzibar na wananchi wake.

Amesema Kamati hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya CCM na ACT Wazalendo, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa na wadau wengine kuendelea kushirikiana katika kujenga Zanzibar yenye amani, utulivu na maendeleo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza viongozi wa CCM, ACT Wazalendo, viongozi wengine wa kisiasa, wazee na Marais Wastaafu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa mchango wao katika kuendeleza mchakato wa maridhiano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema chama hicho kiko tayari kuendelea kushirikiana katika kuijenga Zanzibar, akimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa hatua mbalimbali alizochukua katika kusimamia mchakato wa maridhiano.Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amekabidhi Hadidu Rejea za Kamati kwa Wenyeviti Wenza, Ndg. Omar Ali Sheikh kutoka ACT Wazalendo na Ndg. Abdi Mahmoud Abdi kutoka CCM Zanzibar.




Chapisha Maoni

0 Maoni