Na. Farida Ramadhani na Saidina Msangi, WF, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa inaendelea kuboresha uandaaji wa mipango na bajeti ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2027/28–2029/30.
Hayo yameelezwa katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma na Mhasibu Mkuu Msaidizi wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Ayubu Banzi, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, wakati akifungua kikao kazi cha Tathmini ya Uandaaji na Utekelezaji wa Bajeti kwa wataalamu wa Mipango na Bajeti kundi la pili kati ya makundi matatu yanayoshiriki mafunzo hayo.
Bw. Banzi alisema kikao hicho ni muhimu kwa kuwa kitatoa fursa kwa washiriki kutoa maoni yatakayotumika kuboresha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa bajeti ya Serikali.
Alisema maoni hayo pia yatasaidia kuboresha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2027/28–2029/30.
Kikao hicho kimewahusisha wataalamu wa masuala ya mipango na bajeti kutoka wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Lengo la kikao hicho ni kuhakikisha kuwa wataalamu wanaendelea kuwa na uelewa na uwezo unaohitajika katika maandalizi, utekelezaji na usimamizi wa mipango na bajeti ya Serikali.


0 Maoni