Na. Bakari S. Machumu - Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amekutana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Afrika Mashariki na Kusini, Ndiamé Diop, ambapo wamejadili namna ya kuharakisha uwekezaji wa kimkakati katika kusaidia mageuzi ya kiuchumi nchini.

Rais Samia ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wake wa muda mrefu na Tanzania, hususan katika sekta za elimu, nishati, miundombinu na kilimo, huku akitaka ushirikiano huo uimarishwe zaidi ili kuendana na vipaumbele vya maendeleo vya muda mrefu vya nchi.

Amesema Tanzania inapoingia katika hatua mpya ya mageuzi, kipaumbele ni kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu unachochea uzalishaji, biashara, uwekezaji na ajira kwa wananchi.

Mazungumzo hayo yamejikita katika Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), uunganishaji wa usafiri na nishati kikanda, kilimo cha kisasa, uvuvi, elimu na ukuzaji wa ujuzi, pamoja na fursa za kuhamasisha uwekezaji kutoka sekta binafsi.

Rais Samia amesema Tanzania ina nafasi ya kimkakati kama lango linalounganisha Afrika Mashariki, Kati na Kusini, akisisitiza kuwa uwekezaji katika reli, bandari, barabara na nishati unapaswa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kufungua fursa mpya za kiuchumi katika ukanda wa kati.

Amesema SGR si reli pekee bali ni ukanda wa kiuchumi unaoweza kuchochea viwanda, kilimo, usafirishaji wa mizigo, uanzishwaji wa miji mipya na biashara ya kikanda, hivyo Tanzania inalenga kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zinazotokana na uwekezaji huo mkubwa.

Kuhusu kilimo, Rais Samia amesisitiza azma ya Tanzania kuelekea kilimo cha kisasa, cha kibiashara na kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi, kikisaidiwa na umwagiliaji, teknolojia, mitambo, uongezaji thamani wa mazao na kuimarishwa kwa masoko.

Viongozi hao pia wamejadili umuhimu wa sayansi, teknolojia, elimu ya ufundi na ukuzaji wa ujuzi katika kuwaandaa vijana wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi unaobadilika kwa kasi.

Kwa upande wake, Diop amepongeza maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania na kuthibitisha dhamira ya Benki ya Dunia kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameeleza kuvutiwa na maendeleo ya Tanzania kupitia Mpango wa Mission 300, hususan juhudi za kuongeza upatikanaji wa umeme na kuimarisha uunganishaji wa nishati kikanda.

Diop pia amepongeza maendeleo katika sekta ya elimu, akieleza kuwa alishuhudia maendeleo hayo Zanzibar, yakiwemo matumizi ya sayansi na teknolojia pamoja na uwekezaji unaolenga kuboresha ujifunzaji na kuwaandaa vijana kwa fursa za baadaye.

Aidha, mazungumzo hayo yameangazia nafasi ya sekta binafsi katika kuleta mageuzi ya Tanzania, huku Diop akieleza nia ya Benki ya Dunia kusaidia Tanzania kujenga mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kukua zaidi, ikiwemo kuhamasisha mitaji binafsi na kusaidia uwekezaji wenye tija katika sekta za uzalishaji na miundombinu.

Viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kubadilisha vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania kuwa uwekezaji wa kimkakati wenye uwezo wa kuharakisha ukuaji wa uchumi, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi.