RAIS SAMIA: Kulinda amani ni kulinda uwekezaji na ajira

 

Na. Bakari S. Machumu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu, akisisitiza kuwa ndiyo msingi wa uwekezaji, ajira na ukuaji wa uchumi nchini. 

Akizungumza leo Ikulu, Dar es Salaam, wakati wa Mkutano Maalum wa Serikali na Sekta Binafsi kuhusu Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Rais Samia amesema rasilimali na mitaji mikubwa haviwezi kuleta maendeleo bila kuwepo mazingira ya amani yanayowapa wawekezaji uhakika na kuwawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao bila hofu. Amesema katika safari ya kuelekea Dira 2050 ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda amani ya nchi kwani kufanya hivyo ni kulinda uwekezaji, biashara, ajira na kasi ya ukuaji wa uchumi. 

Rais Samia pia ameitaka sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira 2050 kwa kuongeza uwekezaji, uzalishaji, huduma, matumizi ya teknolojia na ubunifu. Amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, huku akihimiza uwekezaji unaounganisha wazalishaji wakubwa na wadogo, biashara kubwa na ndogo pamoja na matumizi ya wataalamu na wazabuni wa ndani. Aidha, amesisitiza ushirikishwaji wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika shughuli za uzalishaji na mnyororo wa thamani wa sekta binafsi. 

Kadhalika, amewataka wafanyabiashara kuongeza uzalishaji katika sekta za kilimo na viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali za nchi, kuzingatia viwango vya ubora na kupanua biashara katika masoko ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Bara la Afrika na dunia. 

Katika mkutano huo, Rais Samia alizindua nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kukabidhi Ufunguo wa Mtazamo Mpya, unaoashiria mwanzo mpya wa ushirikiano wa uwazi na uaminifu kati ya Serikali na sekta binafsi. Pia ameielekeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuhakikisha elimu kuhusu nyenzo hizo inawafikia wadau wote ili waelewe wajibu wao katika utekelezaji wa Dira hiyo. 

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa Dira 2050, akitaja uwekezaji, sayansi, teknolojia, uchumi wa kidijitali, uchumi wa buluu na maendeleo ya rasilimali watu kuwa maeneo muhimu ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. 

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema mageuzi yaliyofanyika katika mazingira ya biashara yameongeza imani ya wawekezaji na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika kuvutia mitaji. Ametaja kuongezeka kwa uwekezaji katika kampuni changa za teknolojia kwenye sekta za fedha, kilimo na nishati safi kuwa ushahidi wa mafanikio ya maboresho hayo. 

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, amepongeza maboresho ya sera, sheria, mifumo ya utawala, uwekezaji na kodi yaliyopanua nafasi ya sekta binafsi katika uchumi. Wawakilishi wa sekta binafsi wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuongeza uwekezaji, matumizi ya teknolojia na ajira, huku wakiiomba Serikali kuendelea kutunga sera zinazotabirika na kufanya mashauriano ya mara kwa mara kuhusu mazingira ya biashara na uwekezaji. 

Katika hatua nyingine, Rais Samia alishuhudia utiaji saini wa Tamko la Pamoja kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira 2050 na kuzitaka taasisi na vyama vilivyosaini tamko hilo kuwaelimisha wanachama wao, kuliheshimu na kulitekeleza kwa vitendo. Aidha, ametunukiwa Tuzo ya Heshima na Sekta Binafsi Tanzania kwa kutambua mchango wake katika kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na kukuza uchumi jumuishi nchini. 

Akihitimisha mkutano huo, Rais Samia amezitaka Serikali na sekta binafsi kuendeleza ushirikiano wa kuaminiana, kuongeza kasi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuhakikisha inaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.



Chapisha Maoni

0 Maoni