MWANASIASA mstaafu na mwekezaji nchini, Freeman Mbowe ameipongeza serikali kwa kukamilisha Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), akitaka nishati hiyo itumike kuchochea uzalishaji na kujenga uchumi mpya badala ya kuishia kuwasha taa.
Mbowe alisema hayo jana wakati wa uzinduzi rasmi wa kituo hicho Rufiji mkoani Pwani, akisema umeme wa uhakika ni msingi wa uchumi na unapaswa kubadili maisha ya Watanzania.
Alisema serikali inapaswa kuelekeza matumizi ya umeme huo katika kuendesha viwanda, kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo hospitali na shule na kuwawezesha wananchi vijijini kutumia nishati katika shughuli za uzalishaji.
“Umeme huu usiende tu kuwasha taa... Umeme huu ulenge zaidi kwenda kuwa ‘source’ (chanzo) ya uzalishaji,” alisema.
Mbowe alisema nishati hiyo inapaswa kuwezesha uchakataji wa mazao ya wakulima katika vijiji, wilaya na mikoa ili kuongeza thamani ya mazao na kipato cha wananchi.
“Nishati inayokwenda kuzalishwa katika Bwawa la Mwalimu Nyerere si nishati ya mtu binafsi, ni nishati ambayo inakwenda kunyanyua uchumi wa nchi,” alisema. Aidha, alitaka serikali iharakishe ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme ili ufikie maeneo yenye mahitaji, akisema kuzalisha umeme mwingi hakutoshi iwapo hakuna njia za kuufikisha kwa watumiaji.
“Umeme huu usibaki katika ‘turbines’(kifaaa cha kuzalisha umeme) za Mwalimu Nyerere, umeme huu usibaki katika gridi ya taifa, umeme huu ukasambae vijijini,” alisema.
Alishauri pia gharama za umeme na kuunganisha huduma hiyo zipunguzwe ili wananchi waweze kutumia nishati kwa uzalishaji, akibainisha kuwa baadhi yao wanashindwa kuunganishiwa licha ya njia za umeme kupita karibu na nyumba zao. Mbowe alisema JNHPP ni mradi wa taifa ambao haupaswi kuhusishwa na itikadi za kisiasa, kwa kuwa manufaa yake ni kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

0 Maoni