Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha programu ya mafunzo ya uanagenzi kama mkakati madhubuti wa kuwajengea vijana stadi za kazi zitakazowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine, hatua inayolenga kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi wa Taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, amesema hayo jana Julai 18, 2026, wakati alipokagua utekelezaji wa mafunzo hayo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Kampasi ya Rukwa.
Waziri Sangu alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewezesha vijana 5,746 kupata mafunzo ya uanagenzi katika vyuo 46 nchini kwa kugharamia ada, bima ya afya, na nauli za mafunzo kwa vitendo.
Uwekezaji huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaokidhi soko la ajira, huku Waziri Sangu akiahidi kuwa kuanzia mwaka 2026, wahitimu wataanza kupatiwa vifaa vya kuanzia kazi ili kuwawezesha kujiajiri mara moja.
Akizungumzia utekelezaji wa programu hiyo mkoani Rukwa, Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Alana Nchimbi, alieleza kuwa mkoa una vyuo viwili vinavyoshiriki, ambavyo ni MUST Kampasi ya Rukwa yenye wanagenzi 154 na Chuo cha Kilimo na Mifugo Laela chenye wanagenzi 120.
Mkuu wa Kampasi ya MUST Rukwa, Prof. Asheri Mwidege, aliongeza kuwa mafunzo hayo yamewawezesha wanagenzi kupata umahiri wa vitendo, ikiwemo ujenzi wa mageti na ukarabati wa hosteli ndani ya chuo, huku akishukuru Serikali kwa kugharamia bima ya afya na nauli kwa asilimia 100, hatua iliyoongeza ari ya vijana. Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mheshimiwa Nyakia Ally Chirukie, alipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uratibu huo ambao umekuwa chachu ya uwezeshaji kwa vijana wa wilaya hiyo.
Wanagenzi wenyewe wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo ambayo yamekuwa suluhisho la changamoto ya ukosefu wa ajira. Digna Sebastian John, mhitimu wa chuo kikuu aliyebadili mwelekeo na kuanza kujifunza ufundi bomba, alibainisha kuwa ujuzi huo unampa uhakika wa kujiajiri.
Kwa upande wake, Ismail William Mbogo, ambaye awali alikuwa akijishughulikia na kilimo cha mpunga katika Bonde la Ziwa Rukwa, alitoa ushuhuda kuwa ndani ya miezi sita pekee amejenga uwezo mkubwa wa ufundi unaomfanya sasa kupata ajira za muda katika vijiji vinavyozunguka chuo hicho.
Ujumbe huu unadhihirisha kuwa programu
ya uanagenzi si tu inatoa ujuzi, bali inabadilisha maisha ya vijana kutoka
kwenye shughuli za kawaida na kuwaweka kwenye mkondo wa wataalamu wanaochangia
moja kwa moja katika maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi.


0 Maoni