Na. Mwandishi Maalumu
Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza amani, umoja wa kitaifa, maridhiano na maendeleo jumuishi, huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Charles Kadonya akieleza kuwa maadili ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela yanaendelea kuwa dira ya kujenga taifa lenye mshikamano kupitia mazungumzo na kuheshimiana.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela 2026 yaliyofanyika Dar es Salaam juzi, Kadonya alisema Tanzania inaendeleza urithi huo kwa kuwekeza katika elimu bora, ujuzi, ubunifu, ujasiriamali na matumizi sahihi ya teknolojia ili kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa na uongozi bora.
Naye Kaimu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Ronald Tran Ba Huy alihimiza jamii kuenzi siku hiyo kwa kujitolea dakika 67 kama ishara ya miaka 67 ya huduma ya Mandela katika kutetea haki za binadamu, usawa na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Balozi wa Afrika
Kusini nchini Tanzania, Noluthando Mayende-Malepe, alisema Mandela atakumbukwa
daima kwa kusimamia maridhiano, utawala bora na amani, akibainisha kuwa
ushirikiano kati ya Tanzania, Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo utaendelea
kuimarisha usawa wa kijinsia na fursa kwa vijana wakati Siku ya Kimataifa ya
Nelson Mandela ikiadhimishwa rasmi kila Julai 18 kuenzi mchango wake mkubwa
katika mapambano ya haki, usawa na uhuru.

0 Maoni