Mjiolojia
kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Abbas Mruma, amesema
Tanzania inaendelea kujijengea nafasi muhimu duniani kutokana na kuwa na
hifadhi kubwa ya madini muhimu ya kimkakati, yakiwemo graphite, lithium na rare
earth elements, ambayo ni nguzo muhimu katika maendeleo ya teknolojia za kisasa
na nishati safi.
Mruma
ameyasema hayo wakati akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Stanslaus Muyungi, alipotembelea banda la
Tume ya Madini katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
(Sabasaba).
Amesema
mahitaji ya madini ya lithium yanaendelea kuongezeka kwa kasi duniani kutokana
na matumizi yake katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, simu za
mkononi, kompyuta mpakato (laptops) na vifaa vingine vya kisasa vya
kielektroniki.
Amefafanua
kuwa nchini Tanzania, madini ya lithium yanapatikana zaidi katika maeneo ya
Dodoma na Ikungi, mkoani Singida.
Akizungumzia
madini ya graphite, Mruma amesema Tanzania ndiyo nchi inayoongoza barani Afrika
kwa kuwa na hifadhi kubwa ya madini hayo, ambayo ni malighafi muhimu katika
utengenezaji wa betri za magari ya umeme pamoja na matumizi mengine mbalimbali
ya viwandani.
Aidha,
amesema Tanzania pia ina hifadhi kubwa ya madini ya rare earth elements katika
Ukanda wa Afrika Mashariki, yanayopatikana katika eneo la Ngualla mkoani Songwe
na Wigu mkoani Morogoro.
Baada ya
kupokea maelezo hayo, Dkt. Richard Stanslaus Muyungi ameipongeza Tume ya Madini
kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu rasilimali za madini na fursa
zilizopo katika sekta hiyo.
Amesema
elimu hiyo ina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu
wa rasilimali za madini, fursa za uwekezaji na nafasi ya sekta ya madini katika
kukuza uchumi na maendeleo endelevu ya Taifa.


.jpeg)
0 Maoni