Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mradi wa Urejeshaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania imewezesha urejeshaji wa hekta milioni 3.3 za ardhi na misitu iliyoharibiwa hadi kufikia mwezi Desemba 2024.
Hayo yamebainishwa Julai 9, 2026 Mkoani Morogoro na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdllah Hassan Mitawi wakati ufunguzi wa warsha ya kujenga uwezo kikosi-kazi cha taifa cha urejeshaji wa mazingira ya ardhi na misitu iliyoharibika.
Amebainisha kuwa Tanzania imebarikiwa utajiri mkubwa wa mifumo ikolojia ambapo takribani hekta milioni 48 ni misitu, ambapo hata hivyo pamoja na wingi wa rasimali hizo kumekuwepo na changamoto za uharibifu wa mazingira, ambapo tafiti zimeonesha kuwa takribani hekari 469,000 za misitu hupotea kila mwaka.
Mitawi amesema urejeshaji wa Ardhi ya Misitu iliyoharibiwa ni sehemu ya ajenda muhimu ya maendeleo endelevu ya Tanzania, kutokana na hatua hiyo Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kisera na kimkakati kwa kushirikiana na wadau.
Amesema mwa juhudi hizo ni utekelezaji wa Mkakati wa AFR100, unaolenga kurejesha hekta milioni 100 za ardhi na misitu iliyoharibika barani Afrika kufikia mwaka 2030 ambapo mkakati huo unachangia malengo ya kidunia ya kurejesha hekari milioni 350 za ardhi na misitu duniani kote.
Amefafanua kuwa katika kuchangia jitihada za kimataifa na malengo ya uhifadhi mazingira kitaifa, mwaka 2018, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliahidi kurejesha hekta milioni 5.2 za maeneo ya ardhi na misitu iliyoharibika kufikia mwaka 2030 chini ya mkakati wa AFRI100.
Kwa mujibu wa Mitawi amesema mwaka 2024 Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia mradi wa Urejeshaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) ilikamisheni Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kufanya tathmini ya utekelezaji wa ahadi hiyo ili kubaini hatua iliyofikiwa.
Ameeleza utekelezaji wa ahadi hiyo inaongozwa na na Mkakati wa Taia wa Urejeshaji wa Ardhi na Misitu iliyoharibiwa (2023–2033); Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2032); Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 -2034) na Programu ya Mageuzi ya Usimamizi wa Mazingira kuelekea Dira2050.
”Nichukue fursa hii kuwajulisha wajumbe wa kikosi-kazi hiki mchukue jambo hili kwa umakini na uzito unaostahili, kwakuwa Serikali na wadau wote wa masuala ya urejeshaji na hifadhi wa mazingira watategemea sana maoni, ushauri na mapendekezo yenu” amesema Mitawi.
Kaimu Meneja wa Vyanzo vya Mbegu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dk Fortunata Senya alisema Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Urejeshaji wa Mandhari ya Misitu wa mwaka 2023–2030 ili kuhakikisha lengo la kurejesha hekta milioni 5.2 linafikiwa.
Alisema mafanikio ya mpango huo hayawezi kupatikana kwa juhudi za Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki mpana wa wadau mbalimbali wakiwamo taasisi za utafiti, sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na wananchi.
Kwa upande wake, Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Joshua Maguzu alisema taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti zinazolenga kubaini aina sahihi za miti zinazofaa kupandwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kulingana na hali ya udongo na tabianchi.
Alisema matokeo ya tafiti hizo yanawasaidia wataalamu na wananchi kuchagua miche inayostawi vizuri katika maeneo husika, hatua inayoongeza mafanikio ya urejeshaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


0 Maoni