Menejimenti na mameneja wa mikoa wa TARURA wapigwa msasa kuhusu kanuni za maadili katika utumishi wa umma

 

Ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kwa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 Menejimenti ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA na Mameneja wa Mikoa wa Wakala huo wamapatiwa mafunzo kuhusu Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma. 

Mafunzo hayo yamefanyika leo katika Ukumbi wa Wizara ya Maji iliyopo Mtumba jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kikao kazi cha siku nne kilichoanza Julai 21, 2026. 

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala huo Bi. Azimina Mbilinyi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha Wajumbe wa Menejimenti na Mameneja wa Mikoa juu ya wajibu wao katika kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa kutekeleza majukumu yao hivyo kuwa chachu katika kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Naye, Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Hassan Kilenza amesema Watumishi wa Umma ndio Msingi mkubwa wa ufanisi na utekelezaji wa majukumu na mipango ya Serikali ya kukuza uchumi, kutoa huduma bora kwa jamii na kulinda amani na utulivu. 

Ameongeza kuwa bila kuzingatia uadilifu malengo ya kitaifa yaliyokusudiwa na Serikali hayatafikiwa kikamilifu. 

Bw. Kilenza amezitaja Kanuni hizo kuwa ni pamoja na kutoa huduma bora, utii Kwa Serikali, Bidii ya kazi na kutoa huduma bila upendeleo. 

kwa mujibu wa Bw. Kilenza, Kanuni nyingine ni kufanya kazi Kwa uadilifu, kuwajibika Kwa Umma, kuheshimu Sheria na matumizi sahihi ya taarifa. 

Awali mada nyingine tatu ziliwasilishwa kwenye kikao kazi hicho ambazo ni Mpango wa Mafunzo wa Wakala, Utekelezaji wa Mirejesho kupitia Mfumo wa e-Mrejesho na Utekelezaji wa PEPMIS Kwa watumishi wa Wakala.





Chapisha Maoni

0 Maoni