WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amewaalika wafanyabiashara
kutoka Ufaransa wawekeze nchini Tanzania kwani ina fursa ya
kutengeneza ajira, kuhamisha ujuzi na kujenga uchumi wa viwanda kwa
faida ya nchi zote mbili.
“Leo tumefanya mjadala wa
kibiashara na sote tumeshuhudia makubaliano yakisainiwa baina ya
Tanzania Private Sector Foundation na International Chamber of
Commerce (ICC). Makubaliano haya siyo tu mkataba wa kawaida bali ni
daraja la kutupeleka kwenye mafanikio makubwa huko mbele,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumatatu, Julai 6, 2026)
wakati akizungumza na washiriki wa mjadala wa kibiashara baina ya
Tanzania na Ufaransa (Tanzania-France Business Roundtable)
uliofanyika kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania jijini Paris,
Ufaransa.
“Kwa hiyo ninawahimiza wafanyabiashara wa
Ufaransa mtumie vyema fursa hii ya kipekee. Maamuzi yatakayofanywa
leo ndiyo yatakayoamua mwelekeo wa sekta za uchumi za kesho kwa nchi
zetu. Wale watakaowekeza nchini Tanzania hivi sasa, hawatakuwa tu
sehemu ya mageuzi ya uchumi wetu, bali watakuwa washirika wa thamani
katika kujenga moja ya uchumi wenye ushindani mkubwa zaidi barani
Afrika kwa vizazi vijavyo.”
Dkt. Mwigulu amesema Ufaransa
inao utaalamu wa hali ya juu na wa kiwango cha kimataifa katika
teknolojia, uhandisi, nishati, miundombinu, viwanda, masuala ya
fedha, na huduma za afya.
“Kwa upande wake, Tanzania inao
utulivu wa kisiasa, nafasi yake ya kijiografia imekaa kimkakati,
inazo rasilimali nyingi za asili, fursa shindani za uwekezaji,
usimamizi thabiti wa uchumi pamoja na nguvukazi ya vijana wengi na
yenye ari kubwa barani Afrika.”
Amesema maeneo hayo yana
nguvu na yanakamilishana kwani katika umoja wake yanajenga fursa za
kipekee za kukuza maendeleo endelevu na ustawi wenye manufaa ya pande
zote mbili.
“Tunapoanza kwa ujasiri kutekeleza malengo ya
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali yetu itaendelea kuwa
thabiti katika kuhakikisha kunakuwepo mazingira yanayotabirika, yenye
uwazi na rafiki kwa biashara, ambapo uwekezaji unalindwa, ushirikiano
unathaminiwa, na mafanikio yanawanufaisha wadau wote,” amesisitiza.
Waziri Mkuu pia alishuhudia utiaji saini wa Hati ya
Makubaliano (MoU) kati ya Chama cha Kimataifa cha Biashara cha
Ufanransa (ICC) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), ambapo
Mtendaji Mkuu wa TPSF, Bw. Deo Massawe alibadilishana hati hiyo na
Naibu Katibu Mkuu wa ICC, Bw. Julian Kassum.
Mapema, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud
Thabit Kombo, aliwaeleza washiriki wa mjadala huo kwamba kitendo
kilichofanyika leo kinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050 ambayo inasisitiza ushiriki wa sekta binafsi kwa
asilimia 70 katika kuchochea maendeleo ya uchumi.
Kwa upande
wake, Rais wa TPSF, Bi. Angelina Ngalula alisema Tanzania ipo katika
nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu cha mageuzi ya uchumi barani Afrika
chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Kwa
miaka mingi, Ufaransa imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika
uwekezaji. Hata hivyo, kwa sasa tunapaswa kuelekeza nguvu zetu katika
kujenga ushirikiano wa muda mrefu utakaokuza uhamishaji wa
teknolojia, kukuza sekta ya utalii, huduma za kifedha pamoja na
uchumi wa kidijitali. TPSF iko tayari kuwezesha ushirikiano huo kati
ya wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa Ufaransa,” alisema.
Baadhi ya kampuni za Ufaransa zilizoshiriki mjadala huo
zinajihusisha na usimamizi wa nishati ya jua (ikiwemo mifumo ya taa
za barabarani), usafirishaji, maji, nishati, ujenzi, viwanda,
mazingira na ufugaji wa viumbe maji (ikiwemo uzalishaji wa mwani wa
baharini). Kampuni nyingine ni waendeshaji wa huduma za satelaiti
wanaotoa suluhisho bunifu kwa huduma za utangazaji wa sauti na picha,
intaneti ya kasi (broadband), huduma za data, usafiri wa baharini na
anga. Aidha, kulikuwa na wazalishaji wa mabomba maalumu yanayotumika
katika sekta ya mafuta na gesi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa
na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde; Waziri wa Nishati, Deogratius
Ndejembi; Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu
wa Tanzania katika UNESCO, Balozi Saidi Othman Yakubu; Mtendaji Mkuu
wa MEDEF International, Bw. Philippe Gautier; Rais wa Baraza la
Biashara la Ufaransa na Afrika Mashariki, Bi. Celine Gouveia; pamoja
na wajumbe kutoka sekta binafsi ya Tanzania na ujumbe wa
wafanyabiashara kutoka Ufaransa.

0 Maoni