Serikali imesema mageuzi yanayoendelea
kutekelezwa katika sekta ya madini chini ya uongozi wa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye
mazingira bora ya uwekezaji barani Afrika, huku ikiwakaribisha
wawekezaji kuwekeza katika utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, uchakataji
na uongezaji thamani wa madini.
Kauli hiyo imetolewa leo,
Julai 8, 2026, na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa,
wakati akifungua Kongamano la Madini lililofanyika katika Ukumbi wa
Dome, ndani ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es
Salaam (DITF), maarufu Sabasaba.
Dkt. Kiruswa amesema
maboresho ya sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa sekta ya madini
yameongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa sekta binafsi, hatua
zilizochochea ongezeko la uwekezaji, ajira na mchango wa sekta hiyo
katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema Tanzania imejaliwa
kuwa na rasilimali nyingi za madini mengi, ikiwemo dhahabu, almasi,
tanzanite, nikeli, kinywe (graphite), nobium, madini adimu (Rare
Earth Elements), pamoja na madini ya viwandani na ujenzi.
Amebainisha kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeweka
msisitizo katika kuimarisha tafiti za kijiolojia kwa kutumia
teknolojia za kisasa ili kufungua maeneo mapya ya
uwekezaji.
“Serikali haiwaaliki wawekezaji kuja kuchimba
madini pekee, bali pia kuwekeza katika tafiti za kijiolojia,
teknolojia za uchenjuaji, uchakataji, uongezaji thamani wa madini na
viwanda vinavyotumia madini kama malighafi,” amesema Dkt.
Kiruswa.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuboresha sheria
na kanuni za madini ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika
mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo kupitia matumizi ya bidhaa na
huduma zinazotolewa na kampuni za wazawa.
Ameongeza kuwa
utekelezaji wa Programu ya Mining for Brighter Tomorrow (MBT)
unaendelea kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum
kunufaika na fursa zinazotokana na sekta ya madini.
Dkt.
Kiruswa amesema kongamano hilo linatarajiwa kufungua fursa mpya za
biashara na uwekezaji, huku akiwakaribisha wadau kushiriki Mkutano wa
Kimataifa wa Madini utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026, katika
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es
Salaam, kwa lengo la kuendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha
uwekezaji wa madini barani Afrika.
Akitoa mada kuhusu
usimamizi wa leseni na biashara ya madini, Mkurugenzi wa Ukaguzi na
Biashara ya Madini wa Tume ya Madini, CPA Venance Kasiki, amesema
Tume inaendelea kusimamia utoaji wa leseni za utafutaji, uchimbaji,
uongezaji thamani na biashara ya madini kwa kuzingatia Sheria ya
Madini, ili kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha
Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Amesema utoaji wa leseni
unazingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo sifa za waombaji, usajili wa
kampuni na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kupokea na
kuchakata maombi.
Ameongeza kuwa wamiliki wa leseni
wanawajibika kutekeleza mipango ya uchimbaji iliyoidhinishwa, kulinda
mazingira, kuajiri na kuwaendeleza Watanzania, pamoja na kutekeleza
wajibu wa uwajibikaji kwa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
CPA
Kasiki amesema Serikali inaendelea kuimarisha utekelezaji wa Kanuni
za Ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content), zinazolenga
kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika usambazaji wa
bidhaa na huduma ndani ya mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Amesema fursa hizo zinajumuisha usafirishaji, ujenzi,
teknolojia, huduma za ulinzi, huduma za chakula na huduma za
kifedha.
Amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa leseni za
madini pamoja na utekelezaji wa Kanuni za Local Content ni nguzo
muhimu katika kuongeza mapato ya Serikali, kuvutia uwekezaji,
kuimarisha viwanda vya uongezaji thamani na kuhakikisha wananchi
wananufaika zaidi na rasilimali za madini.
Vilevile,
amewahimiza Watanzania kutumia fursa zinazopatikana katika sekta ya
madini kwa kuwekeza katika viwanda vinavyozalisha bidhaa na vifaa
vinavyotumika migodini pamoja na kutoa huduma mbalimbali
zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji na uongezaji thamani wa
madini.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed
Jumanne, amesema sekta ya madini imeendelea kutoa ajira kwa maelfu ya
vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi wa maeneo yenye shughuli za
uchimbaji.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano
katika masuala ya ulinzi na usalama ili shughuli za uchimbaji
zifanyike kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo, hatua
itakayochochea maendeleo endelevu ya sekta hiyo na kuongeza mchango
wake kwa uchumi wa Taifa.



.jpeg)
0 Maoni