Vyama vya siasa nchini vimehimizwa kuzingatia maridhiano yanayosimamiwa na Watanzania wenyewe pasipo kutegemea msaada au ushawishi kutoka mataifa ya nje.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ali Khatib, aliyasema hayo mjini Morogoro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wa baraza hilo.
Khatib, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha ADA-TADEA, alieleza kuwa maridhiano ya dhati hufanywa na viongozi wenye serikali kwa sababu ndio wenye mamlaka ya Bunge na dola, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fikra hiyo chanya inayojenga nchi kwa maslahi mapana ya wananchi.
Katika mazungumzo yake, Khatib aliwakumbusha wanasiasa kuachana na siasa za kuwagawa wananchi na badala yake wajikite katika kujenga umoja, huku akisisitiza kuwa hoja za maridhiano hazipaswi kutumika kama mtaji wa kisiasa.
Aliongeza kuwa baraza hilo limepanga kuishauri serikali kupitia upya suala la zuio la mikutano ya hadhara ili vyama ambavyo havina makosa visiadhibiwe kutokana na makosa ya chama kimoja. Mtazamo huu ulitolewa wakati serikali kupitia Msemaji Mkuu wake, Gerson Msigwa, ikieleza kuwa zuio hilo litaendelea hadi vyombo vya ulinzi na usalamaakapojiridhisha na hali ya amani.
Wakati huohuo, uchaguzi wa viongozi wa baraza hilo ulimrejesha Juma Ali Khatib kuwa mwenyekiti kwa miaka mingine miwili baada ya kujinyakulia kura 30 kati ya 31 zilizopigwa, huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikichukuliwa na John Mongella ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara aliyetetea nafasi yake kwa idadi hiyo hiyo ya kura.
Viongozi wengine kama Katibu Mkuu wa UDP, Saum Rashid, na Mwenyekiti wa AAFP, Said Sudi Said, walitumia fursa hiyo kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kulinda amani, kudumisha utulivu, na kutatua changamoto zote za kitaifa kupitia mazungumzo ya ndani bila kuhusisha nguvu za nje.

0 Maoni