Vijana Watakiwa Kulinda Amani kwa Mustakabali wa Taifa

 

Wadau wa masuala ya uchambuzi wa Afrika pamoja na baadhi ya wanasiasa wamewataka vijana kuwa makini katika mustakabali wa nchi zao, wakisisitiza umuhimu wa kulinda amani na kuepuka hatua zinazoweza kuirejesha jamii katika umaskini na kudhoofisha maendeleo ya taifa.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa makala maalum kuhusu matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025, iliyotayarishwa na mwandishi wa habari kutoka Nigeria, David Hundeyin, katika ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akizungumzia makala hiyo, mwanasiasa mkongwe Hamad Rashid amesema vijana wanapaswa kutambua thamani ya taifa lao na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu taswira ya nchi.

Amesema Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha ajira kwa vijana, akibainisha kuwa suala la ajira ni la kitaifa na linahitaji kushughulikiwa na taasisi zote ili kulinda amani na utulivu.

“Kwenye makala hii nimejifunza umuhimu wa kulinda amani ya nchi na Afrika kwa ujumla. Kama kuna changamoto za haki za binadamu, zishughulikiwe kwa kufuata taratibu sahihi ikiwemo mijadala ya Katiba mpya,” amesema Rashid.

Naye Katibu wa Chama cha NRA, Almas Kisbya, amesema vijana wanapaswa kuwa makini katika kufanya maamuzi na kuthamini rasilimali za taifa lao.

“Vijana wanapaswa kujenga imani kwa taarifa zinazotolewa ndani ya nchi badala ya kutegemea taarifa kutoka nje pekee. Ni muhimu kuthamini taifa letu na kushiriki katika kulijenga,” amesema Kisbya.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya Afrika, Joshua Maponga, amesema vijana wako katika hatari ya kupoteza mwelekeo iwapo hawatakuwa makini.

“Baadhi ya mataifa ya Magharibi hunufaika na hali ya misukosuko katika mataifa ya Afrika, hivyo vijana wanapaswa kuwa makini na kulinda maslahi ya nchi zao,” amesema Maponga.


Chapisha Maoni

0 Maoni