Vijana mkoani Kilimanjaro wamemshukuru kwa dhati Rais Samia Suluhu Hassan kwa programu mbalimbali za uwezeshaji wa kiuchumi zinazotekelezwa na serikali yake, huku wakitoa somo zito kwa vijana wenzao nchini kuacha tabia ya kufuata mikumbo na kulalamika kwenye mitandao ya kijamii bila kuchukua hatua za makusudi kufuatilia fursa zilizopo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, vijana hao wamebainisha kuwa serikali ina nia thabiti ya kuwakomboa vijana kiuchumi, na kwamba siri ya mafanikio ipo katika utayari wa kufuatilia taratibu rasmi, kuwa wabunifu na kuacha maneno ya uongo yanayorudisha nyuma jitihada za maendeleo.
Ukweli
huo unadhihirishwa na mafanikio makubwa ya kikundi cha Quality
Printing kutoka Kata ya Mawenzi katika Manispaa ya Moshi, ambao ni
mfano hai wa jinsi ufuatiliaji kistaarabu na uhakika unavyolipa.
Kikundi hicho kilichoanza mwaka 2020 na kupata usajili rasmi
mwaka 2021 kikiwa na wanachama watano, wakiwemo wanawake wawili na
wanaume watatu, kimepata nafasi ya kuaminiwa na Halmashauri kupitia
mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa maelekezo ya Rais Samia
kuwafikia vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu.
Katika awamu ya kwanza mwaka 2022, kikundi hicho kiliomba na kufanikiwa kupata mkopo wa shilingi milioni 18, na kwa nidhamu kubwa ya kifedha walifanya kazi kwa bidii na kufanikiwa kurejesha fedha hizo kikamilifu hadi kufikia mwaka 2023. Baada ya uaminifu huo, walitulia na kujipanga tena ambapo katika awamu ya pili waliiomba Manispaa na kufanikiwa kupata shilingi milioni 105 mwaka 2025, na kufanya jumla ya uwezeshaji walioupata kufikia shilingi milioni 123 ambao umewasaidia kumiliki ofisi nzuri, kununua mashine za kisasa kabisa, na kutoa huduma bora za uchapishaji.
Mbali
na Quality Printing, vijana wengine walioamua kuchakarika na kuachana
na propaganda za vijiweni ni pamoja na kikundi cha B5 Enterprises
Group, ambao nao wamepata mkopo wa shilingi milioni 43 uliowawezesha
kuonesha njia katika sekta ya kidigitali mtandaoni.
Ushuhuda wa
vikundi hivi unathibitisha kuwa serikali iko kazini na iko tayari
kutoa mitaji ya kuanza maisha kwa vijana wote nchini walio tayari
kujiajiri, na unaleta picha halisi kuwa wanaolalamika mara nyingi
hawajawahi hata kufika kwenye ofisi za halmashauri zao kufuatilia
fursa hizi adimu.
Kufuatia mafanikio hayo, wanakikundi hao wametoa wito kwa vijana wenzao kuweka malengo sahihi, kuwa wabunifu, na kuitumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta mabadiliko ya kweli kwenye maisha yao badala ya kutegemea ajira pekee. Wamesisitiza kuwa wanatambua na kuthamini mchango wa Rais Samia kiongozi mlezi mwenye maono makubwa na wanakuahidi kuifanyia kazi mikopo hiyo kwa ufanisi mkubwa ili kukuza mitaji yao na kutoa ajira kwa vijana wengine, wakisema kuwa wao wapo kazini na Mama kwa ajili ya maendeleo ya uhakika ya Taifa.

0 Maoni