Na. Mwandishi Wetu- Seoul
Fursa za utalii wa misitu na uwekezaji katika
miundombinu ya utalii ndani ya misitu ya hifadhi inayosimamiwa na
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zimetangazwa katika
Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Seoul International Travel Fair
(SITF) 2026 yanayoendelea jijini Seoul, Korea Kusini.
Ushiriki
huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania
(TTB) za kupanua masoko ya utalii katika eneo la Mashariki ya Mbali
na bara la Asia, ambalo linaendelea kuwa miongoni mwa masoko yenye
ukuaji mkubwa wa watalii duniani.
Akizungumza katika maonesho
hayo, Mhifadhi Someni Mteleka wa TFS alisema ushiriki wa Tanzania
unatoa fursa ya kutangaza vivutio vya utalii wa misitu vilivyopo
nchini pamoja na kujifunza mahitaji na matarajio ya watalii wa
kimataifa.
Alisema idadi kubwa ya washiriki wa maonesho hayo
wameonesha kuvutiwa na utalii wa mazingira asilia na kueleza nia ya
kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya misitu
nchini.
“Tumeshuhudia watu wengi wakivutiwa na utalii wa
mazingira asilia na kuonesha hamu ya kutembelea maeneo mbalimbali ya
misitu nchini Tanzania, ikiwemo Mlima Rungwe, Maporomoko ya Kalambo,
Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Amani, Milima ya Magamba, Msitu wa
Chome na Mlima Hanang. Fursa hii pia inatuwezesha kujifunza matarajio
yao ili tuendelee kuboresha huduma na miundombinu ya utalii
ikolojia,” alisema.
Kwa mujibu wa Mteleka, Korea Kusini ni
miongoni mwa nchi zilizofanikiwa kuendeleza utalii wa mazingira
asilia unaojumuisha misitu, milima, maziwa, mito, mabwawa na
maporomoko ya maji, hali inayofanana kwa kiasi kikubwa na utajiri wa
vivutio vilivyopo Tanzania.
Alisema uzoefu unaopatikana
kupitia maonesho hayo utaisaidia Tanzania kuimarisha mipango ya
kuendeleza utalii wa misitu kama zao jipya la utalii lenye mchango
mkubwa katika ukuaji wa uchumi na ajira.
“Tutatumia uzoefu
huu kujenga uwezo wetu katika kuendeleza miundombinu na huduma
zinazowezesha utalii wa misitu kukua na kuchangia zaidi katika uchumi
wa nchi. Hii itasaidia kufanikisha azma ya Serikali ya kufikia
watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030 sambamba na utekelezaji wa
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema.
Korea Kusini
imeendelea kuwa mfano wa mafanikio katika maendeleo ya utalii wa
mazingira asilia, jambo linalofungua fursa kwa Tanzania kujifunza
mbinu bora za usimamizi wa vivutio, huduma za wageni na uwekezaji
katika miundombinu ya utalii wa ikolojia.
Maonesho ya SITF
2026 huwakutanisha wadau wa sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali
duniani, wakiwemo wawekezaji, waendeshaji wa biashara za utalii,
wanunuzi na wauzaji wa huduma za utalii, kwa lengo la kukuza
ushirikiano na biashara katika sekta hiyo.



0 Maoni