Tanzania imeendelea kupanua wigo wa
ushirikiano wa kimataifa katika Sekta ya Madini baada ya Timu ya
Wataalam kutoka Wizara ya Madini ikiongozwa na Kamishina Msaidizi wa
Madini anayesimamia Uongezaji Thamani wa Madini, Mhandisi Modest
Apolinary, kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Al Mansour
Group, Mhe. Sheikh Mansour Bin Jabour Bin Jassim Al Thani, ambaye pia
ni Mwanafamilia wa Kifalme wa Qatar.
Mazungumzo hayo
yaliyofanyika Juni 1, 2026 yalilenga kujadili fursa za uwekezaji na
maeneo ya ushirikiano katika Sekta ya Madini nchini Tanzania, ikiwa
ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuvutia uwekezaji wa
kimkakati kufuatia ziara ya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde,
aliyoifanya nchini Qatar mwezi Februari 2026.
Katika kikao
hicho, pande zote mbili zilijadili fursa mbalimbali za uwekezaji
katika mnyororo wa thamani wa madini, hususan madini muhimu na ya
kimkakati. Kampuni ya Al Mansour Group ilionesha nia ya kuwekeza
katika shughuli za uongezaji thamani wa madini ya dhahabu, nikeli,
kobalti na chuma, hatua inayokwenda sambamba na mkakati wa Tanzania
wa kuongeza thamani ya rasilimali zake kabla ya kuuzwa katika masoko
ya kimataifa.
Majadiliano hayo pia yalihusisha uwezekano wa
ushirikiano katika utengenezaji na usambazaji wa mitambo pamoja na
vifaa vinavyotumika katika shughuli za utafiti, uchorongaji,
uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Kutokana na dhamira hiyo,
ilikubaliwa kuwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lifanye
tathmini ya mahitaji ya wachimbaji wadogo ili kubaini aina ya vifaa
vinavyohitajika kwa lengo la kuimarisha shughuli za utafiti na
uchimbaji nchini.
Aidha, pande hizo mbili zilijadili fursa za
ushirikiano katika mafunzo na kubadilishana uzoefu kwa wataalamu wa
sekta ya madini, hususan katika maeneo ya utafiti wa madini,
teknolojia za uchorongaji, usimamizi wa miradi na elimu ya fedha.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kitaalamu na kuimarisha
ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya madini nchini.
Katika
hatua nyingine, majadiliano yaligusia uwekezaji katika uzalishaji wa
mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana Tanzania. Hatua hiyo
inalenga kuongeza upatikanaji wa mbolea, kupunguza gharama za
uzalishaji kwa wakulima na kuchangia ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja
na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Akizungumza katika
kikao hicho, Mhandisi Modest Apolinary alisema Wizara ya Madini ipo
tayari kushirikiana na Al Mansour Group katika maeneo mbalimbali ya
utafiti, uchimbaji, uongezaji thamani wa madini na maendeleo ya
rasilimali watu ili kuhakikisha pande zote zinanufaika na ushirikiano
huo.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe.
Habibu Mohamed, alisema Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa maeneo
bora ya uwekezaji kutokana na mazingira yake tulivu, sera rafiki za
uwekezaji na mifumo ya kisheria inayolinda mitaji ya
wawekezaji.
‘’Tunaikaribisha Al Mansour Group kuwekeza
nchini Tanzania na kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya
Madini, Viwanda na Kilimo,” alisema Balozi Habibu.
Naye,
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt.
Venance Mwasse, alisema shirika hilo liko tayari kushirikiana na
kampuni hiyo katika maeneo yote ambayo imeonesha nia ya kuwekeza,
akibainisha kuwa ushirikiano huo utaongeza uwekezaji, kuhamasisha
matumizi ya teknolojia za kisasa, kuimarisha shughuli za utafiti na
uchimbaji wa madini pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya madini
katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mazungumzo hayo ya wataalam
kutoka Wizara ya Madini, STAMICO na kampuni hiyo yanaashiria hatua
mpya katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na
Qatar, huku yakifungua fursa za uwekezaji, teknolojia na uongezaji
thamani wa rasilimali madini kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.
Aidha, timu hiyo inatarajia kukutana na Kampuni mbalimbali za uwekezaji.
#InvestInTanzania
#MiningSector
#MineralForGrowth
#StrategicMinerals
#ValueAddition
#TanzaniaQatarPartnership


0 Maoni