Maabara ya kisasa yenye uwezo wa kutoa majibu ya uchunguzi wa shambulio la moyo (Cardiac Troponin Test) ndani ya dakika nane imetajwa kuwa mwarobaini katika kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo.
Maabara hiyo ya kidigitali iliyopo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni miongoni mwa maabara kubwa zaidi Afrika Mashariki na kati ikiwa na uwezo wa kuchakata sampuli nyingi kwa muda mfupi kwa kutumia tekinologia ya kisasa yenye kiwango kidogo cha kumshirikisha mwanadamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema uwekezaji huo mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani umepunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo kwa wagonjwa kutoka saa tatu hadi saa moja na dakika nane.
"Maabara hii imekuwa kivutio kikubwa kwa nchi mbalimbali za Afrika kutokana na matumizi ya tekinologia ya hali ya juu inayowezesha uchakataji wa sampuli nyingi kwa wakati mmoja na kutoa majibu kwa usahihi mkubwa ambapo hali hii inalenga kuboresha huduma na kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo", alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema baada ya uzinduzi wa maabara hiyo JKCI imetoa fursa kwa hospitali mbalimbali kutoka mikoa sita pamoja na Zanzibar kujifunza kuhusu teknologia mpya ya maabara za kidigitali zinazotumia akili unde.
"Wataalamu wetu wa maabara watakuwa katika viwanja vya JKCI kwa muda wa siku tano wakitoa mafunzo kwa wakuu wa maabara kutoka maeneo mbalimbali kubadilishana uzoefu na kupata ujuzi utakaowasaidia kupunguza changamoto za wagonjwa kusubiri majibu ya vipimo kwa muda mrefu", alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo Cha Maabara wa JKCI Thadei Kavishe alisema uzinduzi wa maabara hiyo unaenda sambamba na wiki ya uhamasishaji wa huduma za maabara ambapo wananchi watapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa malaria na mafuta kwenye damu bila malipo.
"Wiki hii tutaonyesha uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika maabara hii ambayo inahakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwani maabara hii pia ina uwezo wa kuchakata sampuli ya malaria na kugundua maambukizi katika hatua za awali tofauti na awali ambapo tulikuwa tunagundua ikiwa hatua ya tatu", alisema Kavishe.
Naye Mkuu wa Kampuni ya Roche Kenya Limited Afrika Mashariki Taofik Oloruko-Oba ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika taasisi hiyo kwa lengo la kuokoa maisha ya watu wenye magonjwa mbalimbali.
"Uwekezaji huu unapunguza hitaji la kupeleka sampuli nje ya nchi kwaajili ya uchunguzi na kupunguza gharama za matibabu ambapo nchini Tanzania takribani watu 5000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na matatizo ya moyo hivyo vifaa hivi vya kisasa vitasaidia kuimarisha uchunguzi na kuokoa maisha ya wananchi wengi", alisema Taofik.
Mmoja wa mwananchi aliyefika kupata huduma za uchuguzi wa malaria na mafuta kwenye damu Mery Magwila ameipongeza Serikali kwa kutoa fursa ya wananchi kufanyiwa uchunguzi bila malipo na kuwapunguzia gharama.
"Naomba huduma hii niliyonufaika nayo iwafikie pia wananchi walioko maeneo ya pembezoni ili waweze kufahamu hali zao za afya mapema na kuchukua hatua stahiki" alisema Mery mkazi wa Dar es Salaam.

.jpeg)
0 Maoni