Kihongosi awataka wananchi Hanang' kuepuka maandamano na vurugu

 

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka wananchi wa Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara kutokubali kushawishiwa kushiriki maandamano ya vurugu, akisema yanaweza kusababisha uharibifu wa mali za umma na kurudisha nyuma jitihada za maendeleo.

Akizungumza katika mkutano na wananchi wa Hanang', Kihongosi alisema watu wanaochochea vurugu hawana maslahi ya wananchi kwa kuwa athari za matukio hayo huwakumba wananchi wenyewe kupitia uharibifu wa huduma muhimu na miundombinu ya kijamii.

Alieleza kuwa vitendo vya kuchoma vituo vya polisi, vituo vya afya na miundombinu mingine ya umma husababisha hasara kubwa kwa jamii na kuathiri utoaji wa huduma muhimu zinazotegemewa na wananchi katika maisha yao ya kila siku.

"Wanaowashawishi kushiriki vurugu hawana maslahi na maendeleo ya wananchi. Mali zinazoharibiwa ni za wananchi wenyewe na madhara yake huwakumba wananchi kwa kupoteza huduma muhimu," alisema Kihongosi.

Kiongozi huyo wa CCM aliwataka wananchi kuelekeza nguvu zao katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

Alisema maandamano yenye tija kwa wananchi ni yale yanayochochea maendeleo kupitia kufanya kazi kwa bidii, kuongeza uzalishaji na kuboresha hali za maisha.

"Maandamano ya maendeleo ni kufanya kazi kwa bidii, kulima, kufanya biashara na kuendesha shughuli halali za kujiongezea kipato. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla," alisema.

Aidha, aliwasisitiza wakulima, wafanyabiashara na waendesha bodaboda kuendelea kujikita katika shughuli zao za kiuchumi huku wakilinda amani na mshikamano wa jamii.

Kihongosi alihitimisha kwa kuwataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kulinda amani ya nchi, akisema utulivu uliopo ni msingi muhimu wa ustawi wa familia na maendeleo ya taifa.

Chapisha Maoni

0 Maoni