WAZIRI
MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Mei 11, 2026 amekutana na Rais wa
Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Alvaro Lario,
jijini Nairobi, Kenya, ambapo wamejadili maeneo mbalimbali ya
ushirikiano katika sekta ya kilimo na uwezeshaji wa wananchi
kiuchumi.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mwigulu amesema
Tanzania itaendelea kushirikiana na IFAD katika maeneo mbalimbali
ikiwemo kilimo himilivu cha tabianchi, maendeleo ya kilimo biashara,
mapinduzi ya kidijitali katika sekta ya kilimo pamoja na uwezeshaji
wa vijana na wanawake kiuchumi.
Aidha, Waziri Mkuu amesema
Tanzania inatarajia kuendelea kushirikiana na IFAD katika utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo ikiwemo mpango wa
kuongeza uzalishaji wa alizeti ili kusaidia kuongeza upatikanaji wa
mafuta ya kula nchini.
“Kimekuwa ni kikao kizuri kwa sababu
tumekuwa na ushirikiano nao kwa muda mrefu, ambapo katika kipindi
kilichopita tumeshirikiana nao katika miradi mbalimbali, na hasa
miradi katika sekta za uzalishaji”.
“Lakini pia
tumedhamiria kuendelea kushirikiana katika kuendeleza mazao ya
mchanganyiko ambayo katika miaka ya nyuma ilikuwa inachukuliwa kuwa
ni mazao ya chakula peke yake, kwasasa mazao haya niya biashara na
tunayafanya sehemu ya kukuza biashara ambayo Tanzania inafanya na
nchi nyingine”
Ameongeza kuwa Tanzania inatarajia kuendelea
kushirikiana na IFAD katika sekta ya mifugo na mazao ya baharini kwa
upande wa Zanzibar.
“Sambamba na hayo, tunategemea
kushirikiana nao katika utekelezaji wa kilimo endelevu ambacho
kinasaidia kampeni yetu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
nchi”. Amesisitiza Dkt. Mwigulu
Kwa upande wa Rais wa IFAD
Alvaro Lario, amesema kuwa wataendelea kuhakikisha mipango na
utekelezaji wa IFAD vinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo ya Tanzania 2050
“Kwasasa tunasubiri kusikia
vipaumbele ya Tanzania ili tujue namna gani tunaweza kusaidia katika
maeneo vya utoshelevu na usalama wa chakula pamoja na uongezaji
thamani wa mazao”



0 Maoni