Kutoka Pemba, Unguja, Mji Mkongwe, Bagamoyo,
Kondoa, Magofu ya Kilwa, paa la Mlima Kilimanjaro na maeneo mengine
ya Tanzania, wadau wa urithi wa dunia wamekutana katika Makumbusho ya
Urithi Geopark Karatu Mkoani Arusha yanayosimamiwa na Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuadhimisha Urithi wa Dunia
Afrika yaliyoanza leo tarehe 04/05/2026 hadi tarehe
05/05/2026.
Wakiwa katika jengo la makumbusho ya Urithi
Geopark Wadau hao wameelezwa jinsi Ngorongoro ilivyo ni utajiri wa
urithi wa dunia kutokana na uumbwaji wake uliotokana na mlipuko wa
volcano zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita na kutengeneza kasoko
iliyokusanya asili, uhai wa binadamu, mifumo ya ikolojia, na ustawi
wa viumbe mbalimbali.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw.
Abdul-Razaq Badru amewashukuru wadau wote hasa Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuipa fursa
Ngorongoro kuandaa na kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kwa mwaka
huu.
Wadau wa urithi wa duania wakiwa katika Makumbusho ya
Urithi Geopark walipata fursa ya kuelezewa kuhusu uthibitisho wa
wasomi unaoeleza wazi historia ya chimbuko la binadamu wa kale
aliyepatikana katika bonde la olduvai takribani milioni 2 iliyopita
na ushahidi wa Nyanyo za binadamu wa kale katika eneo la Laetoli
takribani miaka 3.6 iliyopiTa ambapo binadamu hao walitembea kwa
miguu miwili.
Taasisi zinazoshiriki maadhimisho hayo ambazo
zinasimamia maeneo ya urithi wa dunia ni pamoja na Mamlaka ya Hifadhi
ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA) Mamlaka ya Uzimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Huduma
za misitu Tanzania (TFS), pamoja na wawakilishi wa maeneo ya urithi
wa dunia kutoka Zanzibar.



0 Maoni