Maridhiano: Njia ya Kusonga Mbele Pamoja kama Taifa

 

Mwalimu Nyerere alisema Tanzania inajengwa juu ya amani, majadiliano, na heshima kwa binadamu. Maridhiano ndiyo njia ya kulinda msingi huo. Sisi sote tumewahi kuumizana na kuumizwa. Katika familia, kazini, kwenye siasa, hata kati ya marafiki, hali hii inatupa wajibu kuwa ili tuendelee kuishi pamoja, tunahitaji kitu kimoja ambacho ni maridhiano.

Maridhiano ni kukubali kilichotokea, kusikiliza maumivu ya mwenzio, na kuchagua kukaa pamoja na kuweka tofauti zetu na kusonga mbele. Hii haina maana kila mtu lazima akubaliane na kila kitu. Maana yake ni kuwa tunaweza kutofautiana, lakini bado tukaheshimiana na kuishi pamoja.
Kwa nini tunahitaji maridhiano?

Ukweli ni kwamba tunahitaji maridhiano kutuponya, tukiweka chuki moyoni kwa miaka mingi, unaumia zaidi wewe mwenyewe. Maridhiano yanafungua nafasi ya kujenga umoja wa kitaifa na mshikamano.
Aidha, maridhiano yanajenga uaminifu, kusikilizana na kuaminiana zaidi. Taifa linaloaminiana linapiga hatua haraka katika Nyanja zote za zinazogusa maisha ya wananchi.

Pia, mariadhiano, yanachangia kuongeza kasi ya ya maendeleo, nchi inayopoteza muda mwingi kwenye mivutano haiwezi kujenga shule, hospitali, wala barabara. Maridhiano yanaongeza kasi ya utekelezaji.
Vitendo vidogo ndivyo vinavyojenga familia imara, jamii imara, na taifa imara. Maridhiano siyo udhaifu. Ni ujasiri wa kusema “tumeshajikwaa, lakini hatutaki kubaki hapo”.

Taifa lenye maridhiano halikosi changamoto, lakini linakuwa na nguvu ya kukabiliana nazo kwa pamoja.Umoja wetu unajengwa kila siku, kwa kila mazungumzo, kwa kila hatua ya kuelewana.

Chapisha Maoni

0 Maoni