MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amesema chama hicho kipo tayari kushiriki midahalo ya kisiasa itakayohusisha vyama mbalimbali nchini.
Wasira aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mahojiano na kituo cha Azam TV, akibainisha kuwa CCM iko wazi kushiriki mijadala hiyo iwapo itaandaliwa kwa utaratibu rasmi.
Alisema waandaaji wa midahalo wanapaswa kuwasilisha mwaliko rasmi kwa chama hicho ili waweze kushiriki kikamilifu.
Alipoulizwa iwapo angekubali kushiriki mdahalo utakaowakutanisha Makamu wenyeviti wa CCM, CHADEMA na ACT-Wazalendo endapo Azam TV itaandaa, Wasira alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mwaliko pamoja na ajenda ya mjadala.
“Wewe waite wote wanaoweza kuja, halafu tuzungumze na utuletee ajenda ili tujue tunakuja kujadili nini,” alisema Wasira.
Akizungumzia midahalo ya wagombea urais, Wasira alieleza kuwa ni muhimu kwa mijadala hiyo kuwa na staha na hoja zenye kujenga, akionya kuwa hatashiriki katika midahalo inayolenga matusi badala ya hoja.
"Kwa mfano ikiwa wewe ni mgombea na wewe hulka yako ni kutukana tu, unategemea mimi nitakuja kutukan?, nikuaacha tu uendelee wewe," alisema Wasira.

0 Maoni