Wananchi wa mkoa wa Njombe wameelezwa kuwa wako tayari kumpokea Rais Samia Suluhu Hassan, anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kitaifa yatakayofanyika katika viwanja vya Lunyanywi mjini Njombe.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, akibainisha kuwa maandalizi ya sherehe hizo yamekamilika kwa kiwango kinachokidhi kumpokea kiongozi mkuu wa nchi.
Mtaka amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu ni: “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”
Ametoa wito kwa wananchi wa makundi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo, akiwemo wakulima, wajasiriamali pamoja na wale wasio na ajira rasmi.
“Wananchi wapo tayari. Walioko mashambani, wajasiriamali na makundi yote, hata wale wasio na ajira rasmi, naomba wajitokeze kwa wingi kushiriki maadhimisho haya. Ni fursa ya kuenzi mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa letu,” amesema Mtaka.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amesema maandalizi ya kumpokea Rais Samia yamekamilika na wana matumaini kuwa hotuba yake itagusa maslahi ya wafanyakazi nchini.

0 Maoni