Wafanyabiashara wa nguo za mitumba katika eneo la Ilala jijini Dar es Salaam, wameeleza jinsi wanavyonufaika na hali ya amani na utulivu uliopo nchini, wakisema mazingira hayo yamekuwa chachu ya kuimarisha shughuli zao za kila siku.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Elihuruma Tuvaku amesema utulivu uliopo unawawezesha kufanya biashara zao bila hofu, hali inayowapa uhakika wa kupata wateja na kuongeza kipato chao. Amesema amani imekuwa nguzo muhimu inayowasaidia kupanga na kutekeleza mipango yao ya kibiashara kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Sadick Zuberi ameeleza kuwa hali ya amani inachangia kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa bidhaa zao, kwani hawalazimiki kuwa na hofu ya uporaji au vurugu zinazoweza kuharibu mali zao. Amesisitiza kuwa utulivu unawapa nafasi ya kuwekeza zaidi na kuboresha biashara zao.
Naye Hosea Ambakile amesema kuwa mbali na amani, umoja uliopo miongoni mwa wafanyabiashara hao umekuwa msaada mkubwa katika kukuza biashara zao.
Wafanyabiashara hao wameongeza kuwa mshikamano wao unawasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika biashara, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya bei na ushindani wa soko, hivyo kuwawezesha kusimama imara na kuendelea kukua.
Kwa pamoja, wametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani na kuenzi umoja, wakisema kuwa mafanikio ya biashara nyingi ndogondogo yanategemea kwa kiasi kikubwa mazingira ya utulivu na ushirikiano uliopo katika jamii.
#SisiNiWamoja

0 Maoni