MAGEREZA ya Ukonga yamepongezwa kwa mafanikio makubwa ya utunzaji wa mazingira baada ya kuonesha mfano bora wa upandaji na uhifadhi wa miti, hatua inayochangia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamishna Mwandamizi wa
Kikosi Maalum cha Magereza Tanzania jana Aprili 24,2026, Hamis Lissu,
alipokutana na maafisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
waliotembelea magereza hayo kufanya tathmini ya miche iliyotolewa na
wakala huo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Lissu alizitaka
taasisi na wananchi kuongeza juhudi za upandaji miti na matumizi ya
nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na rasilimali za
taifa.
Alisema utunzaji wa mazingira si jukumu la serikali
pekee bali ni wajibu wa kila mmoja, akisisitiza kuwa hatua za sasa
ndizo zitakazoamua mustakabali wa mazingira kwa vizazi vijavyo.
Kwa
mujibu wa Lissu, miti iliyopandwa katika Magereza ya Ukonga
imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya hewa, kupunguza joto
na kuongeza mvuto wa mazingira ya eneo hilo.
Kwa upande wake,
Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Happiness Kivuyo, alisema taasisi hiyo
imeridhishwa na namna magereza hayo yalivyotunza miche
waliyopewa.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa TFS Kanda ya
Mashariki, SACC Mathew Ntilicha, Kivuyo alisema miti mingi imekua
vizuri na inaonesha usimamizi makini wa mazingira.
Alibainisha
kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya TFS na
taasisi za umma katika kusimamia rasilimali za misitu.
Aidha,
aliwataka wadau wengine kuiga mfano huo kwa kuchukua miche kutoka TFS
na kuipanda ili kuongeza uoto wa asili na kukabiliana na uharibifu wa
mazingira.
Hatua ya Magereza ya Ukonga imeelezwa kuwa mfano
bora wa kuigwa kitaifa, huku wataalamu wakisisitiza kuwa juhudi za
pamoja ndizo zenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kudumu katika
uhifadhi wa mazingira.



0 Maoni