Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kuandikishwa jeshini kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu kuanzia sekondari hadi elimu ya juu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Luteni Kanali Kevin Baraka Byabato, vijana watakaochaguliwa kujiunga na jeshi watapatiwa mafunzo mbalimbali ya kijeshi pamoja na mafunzo yatakayowawezesha kujiendeleza kitaaluma.
Amesema waombaji wanapaswa kukidhi vigezo kadhaa, ikiwemo kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, na kuwa na umri usiozidi miaka 25 kwa wenye elimu ya kidato cha nne na sita, huku kwa wenye elimu ya juu umri usizidi miaka 28.
Aidha, mwombaji anatakiwa kuwa na afya njema ya mwili na akili, kuwa na tabia njema na nidhamu, pamoja na kutokuwa amewahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai mahakamani au kufungwa.
Kwa upande wa nyaraka, waombaji wanatakiwa kuwa na cheti halisi cha kuzaliwa pamoja na vyeti vya masomo vilivyothibitishwa.
Vilevile, mwombaji hapaswi kuwa amewahi kutumikia katika vyombo vya ulinzi na usalama kama vile Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo au taasisi nyingine zinazofanana na hizo.
Pia, imeelezwa kuwa mwombaji anapaswa kuwa amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mkataba wa kujitolea kwa muda wa miaka miwili au kwa mujibu wa sheria na kutunukiwa cheti husika.
Maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi, Msalato Dodoma kuanzia tarehe 15 Aprili, 2026 hadi tarehe 28 Aprili, 2026, yakiwa na viambatanisho vifuatavyo:-
Nakala ya Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA, nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo pamoja na nakala ya cheti cha JKT kwa waombaji waliomaliza mkataba.
Taarifa hiyo ya Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Luteni Kanali Kevin Baraka Byabato, imehitimisha kwa kusema kwamba vijana waliopo kwenye makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hawahusiki na tangazo hili.

0 Maoni