Aliyekuwa mgombea nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka 2025 kupitia chama cha siasa cha NLD, Doyo Hassan, amewataka Watanzania kuacha mara moja kuwatukana na kuwakejeli wajumbe wa tume iliyofanya uchunguzi wa matukio wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, baada ya kuwasilisha ripoti yao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Aprili 23, 2026.
Amesema ni muhimu kwa wananchi kuheshimu kazi iliyofanywa na Tume hiyo pamoja na wajumbe wake, akisisitiza kuwa walitekeleza jukumu lao kwa mujibu wa sheria na kwa maslahi ya taifa zima, hivyo hakuna sababu yoyote ya kuwatukana “kwanza wale ni wazee wetu”.
Doyo alieleza kuwa vitendo vya matusi na kejeli vinaweza kudhoofisha juhudi za kutafuta ukweli na haki, huku vikichochea mgawanyiko usio wa lazima miongoni mwa wananchi.
Aidha, amewahimiza Watanzania kuwa wavumilivu na kusubiri utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti hiyo, badala ya kutoa hukumu za haraka au kueneza taarifa zisizo sahihi.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi, pamoja na viongozi wa kisiasa, kulinda amani na mshikamano wa kitaifa kwa kuheshimu taasisi za kisheria na kuendeleza mjadala wenye staha na unaolenga kujenga taifa.
Hapo jana mjumbe wa tume hiyo, Profesa Ibrahim Juma, alisema Tanzania kumezuka tabia hatari ya watu kuzima maoni ya wengine, huku wakitaka ya kwao pekee ndio yasikilizwe.
Tabia hiyo, amesema imedhihirika hata baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya tume hiyo, baadhi ya wajumbe wamepokea jumbe zaidi ya 300 za matusi katika simu zao, kutoka kwa watu hao ili kuzima maoni yaliyowasilishwa kupitia ripoti.
Profesa Juma, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam Jumanne Aprili 28, 2026 alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari, katika mkutano ulioitishwa na tume hiyo kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali ya kwenye ripoti ya tume.

0 Maoni