Amani Ni Msingi wa Biashara ya Bodaboda - Waendesha Boda Madale

Waendesha bodaboda wa Madale jijini Dar es Salaam wameeleza kuwa amani na utulivu ni nguzo muhimu katika kuhakikisha shughuli zao za kila siku zinafanyika kwa ufanisi na kuleta kipato halali.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bariki Lema amesema kuwa bila uwepo wa amani, kazi ya bodaboda hukumbwa na changamoto nyingi ikiwemo hofu ya usalama wa dereva na abiria, jambo linaloweza kudhoofisha biashara hiyo.

Kwa upande wake, Salehe Kijoti amebainisha kuwa utulivu wa nchi unawapa nafasi waendesha bodaboda kufanya kazi zao kwa uhuru na kuwahudumia wananchi kwa uaminifu, huku akisisitiza kuwa vurugu huathiri moja kwa moja kipato chao cha kila siku.

Naye Rashid Said amesema kuwa ni muhimu kwa vijana, hususan waendesha bodaboda, kuwa walinzi wa amani kwa kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa sheria, akiongeza kuwa usalama wa taifa huanza na mtu mmoja mmoja.

Richard Samweli ametoa wito kwa waendesha bodaboda wenzake kutokubali kushawishika kujiingiza katika vitendo vya fujo, vurugu au uhalifu, akisema kuwa kufanya hivyo kunaweza kuharibu mustakabali wao na kuleta athari kwa jamii nzima.

Kwa pamoja, wamewahimiza vijana wengine nchini kuendelea kuthamini amani na utulivu uliopo, wakisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana pale ambapo jamii inaishi kwa mshikamano, kuheshimiana na kufuata sheria za nchi.

#SisiNiWamoja

Chapisha Maoni

0 Maoni