SMZ imewekeza kiasi kikubwa miundombinu ya michezo na akademia

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika kuimarisha miundombinu ya viwanja vya michezo na akademia za michezo ili kuinua sekta hiyo nchini. 

Amesema Serikali ina dhamira ya kuona michezo yote inaimarika na kupata maendeleo makubwa, na ipo tayari kushirikiana na wadau ili kufanikisha hilo kupitia mipango bora na endelevu. 

Aidha, ameihakikishia Taasisi ya Tanzania Securities Limited kuwa Serikali itashirikiana nayo katika kutekeleza wazo la kukuza mpira wa miguu, ikiwemo kuongeza thamani ya vilabu, kuboresha maslahi ya wachezaji pamoja na kuwajengea mazingira ya kutambua thamani yao. 

Rais Dkt. Mwinyi pia ameishauri taasisi hiyo kuweka mkazo katika kuvijengea uwezo vilabu na vyama vya michezo katika masuala ya uongozi na uendeshaji, akibainisha kuwa ukosefu wa uongozi bora ni moja ya changamoto kubwa katika sekta ya michezo hususan soka. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Securities Limited, Ndg. George Shumbusho, amesema taasisi hiyo imejipanga kuiongezea thamani Ligi Kuu ya Zanzibar ili iwe chombo muhimu cha kuitangaza Zanzibar kimataifa. 

Amesema pia wana mpango wa kuanzisha mfuko wa uwekezaji katika mpira wa miguu pamoja na kuwajengea wachezaji uelewa wa masuala ya fedha ili kuwaandaa kwa maisha baada ya kustaafu.





Chapisha Maoni

0 Maoni