RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kuijalia nchi amani zaidi.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 06 Machi 2026, alipojumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika ibada ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti wa Utheymin uliopo Mbweni kwa Jastuma, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa majanga ya vita yanayoendelea katika nchi nyengine, akitolea mfano mzozo wa Mashariki ya Kati, yanatokana na kukosekana kwa maelewano na amani.
Ameeleza kuwa majanga hayo yamekuwa yakiathiri nchi mbalimbali duniani kiuchumi na kijamii.
Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema ni vema kwa waumini kuendelea kuiombea amani Zanzibar, kwani bila ya amani hakuna jambo lolote la maendeleo linaloweza kufanyika.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amewanasihi Waumini wa Dini ya Kiislamu kuongeza juhudi katika kutekeleza ibada wakati huu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ukiwa katika kumi la pili.

.jpeg)
.jpeg)
0 Maoni