Rais Dkt. Mwinyi aihimiza KCB kushirikiana na SMZ kuwawezesha vijana

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameihimiza Benki ya KCB Tanzania kupitia programu yake ya kurudisha fadhila kwa jamii kushirikiana na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji kutafuta njia bora na endelevu za kuwawezesha vijana, hususan katika upatikanaji wa mikopo ili waweze kujiajiri. 

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa KCB Tanzania, Ndg. Cosmas Kimario, pamoja na Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Peter Kallaghe, wakiongozana na watendaji wakuu wa taasisi hiyo waliofika Ikulu, Zanzibar. 

Dkt. Mwinyi ameishauri Benki ya KCB Tanzania kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa bandari, viwanja vya ndege na miundombinu ya barabara inayohitaji rasilimali kubwa za kifedha ili kukamilika kwa wakati. 

Vilevile, ameihakikishia KCB kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mpango madhubuti wa kulipa mikopo kupitia akaunti maalum inayotumika katika kugharamia miradi ya maendeleo. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa KCB Tanzania, Ndg. Cosmas Kimario, amesema mazingira mazuri ya uwekezaji Zanzibar, maendeleo ya miundombinu pamoja na mkazo katika sekta za uchumi wa buluu na utalii yameivutia benki hiyo kuongeza mtaji wake kwa ajili ya Zanzibar na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.



Chapisha Maoni

0 Maoni