UPINZANI NA MAENDELEO: Mbunge Ado afungua ukurasa mpya kutekeleza dira ya 2050 Tunduru

Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kupitia chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu Ado, amesisitiza kuwa nafasi ya upinzani nchini si kupinga maendeleo, bali ni kushirikiana na wananchi katika kutekeleza kwa vitendo Dira ya Taifa ya 2050.

Mbunge huyo amebainisha kuwa lengo kuu ni kujenga uchumi jumuishi na wenye ushindani kuanzia ngazi ya chini, huku akitangaza azma ya kuibadilisha sura ya Kata ya Matemanga iliyopo Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kwa kuweka kipaumbele katika miundombinu ya msingi.

Akizungumza mbele ya wananchi wa jimbo lake, Ado amesema amejipanga kuhakikisha wakazi wa Tunduru wanatumia rasilimali walizonazo kama ardhi, madini, mbuga za wanyama na mazao ya kilimo ili kujikwamua kiuchumi. Amesema kuwa nguvu kazi ya watu wa Tunduru na hali nzuri ya hewa ni nyenzo muhimu zinazopaswa kuoanishwa na mipango ya kisasa ya maendeleo ili kuleta mageuzi ya kweli yanayoendana na hadhi ya kihistoria ya maeneo hayo.

Katika kuelekea mabadiliko hayo, Mbunge Ado ameanika vipaumbele vitatu makuu atakavyovipigania ndani ya kipindi cha miaka mitano ili kuufanya mji wa Matemanga kuchangamka kiuchumi. Vipaumbele hivyo ni pamoja na ujenzi wa stendi rasmi ya magari ya abiria, ujenzi wa stendi ya malori, pamoja na uanzishwaji wa soko la kisasa. Ameeleza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo ndiyo msingi wa kuufungua mji, kuvutia wawekezaji na kuongeza mzunguko wa fedha kwa mwananchi mmoja mmoja.

Pia, Mbunge huyo amewahakikishia wananchi kuwa utekelezaji wa miradi hiyo hautakuwa wa kutoa amri kutoka juu, bali utazingatia ushirikishwaji wa karibu wa wakazi wa eneo hilo. Amesema hatachukua maamuzi yatakayokwenda kinyume na maslahi ya wananchi, akiamini kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana pale sauti za walengwa zinaposikilizwa. Hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za Kitaifa za kufikia uchumi imara ifikapo mwaka 2050 kupitia ushirikiano wa wadau wote wa siasa na jamii.

Chapisha Maoni

0 Maoni