Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetoa wito mzito kwa wazawa kuacha kusikiliza sauti za kukatisha tamaa na badala yake wajikite katika kuwekeza ndani ya nchi, ikitolea mfano mradi wa kihistoria wa City Park Garden jijini Mbeya uliogharimu Shilingi Bilioni 8.
Katika ziara ya uhamasishaji iliyofanyika Februari 16, 2026, Meneja Uhamasishaji wa TISEZA, Bw. Daudi Riganda, amebainisha kuwa mradi huo unaomilikiwa na kampuni ya kizalendo ya BABITO Trading, ni dhihirisho tosha kuwa Mtanzania anaweza kufanya makubwa ikiwa atatumia vivutio vinavyotolewa na Serikali.
Mradi huo umefanikiwa kupata punguzo la ushuru wa forodha kwa asilimia 75 kwenye vifaa vya uzalishaji, jambo ambalo ni fursa ya wazi kwa mzawa yeyote.
Licha ya uwekezaji huo kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa vijana 100 na kuimarisha sura ya Jiji la Kijani, kumeibuka mjadala miongoni mwa baadhi ya wananchi wanaotia shaka thamani ya mradi huo. Hata hivyo, wachambuzi wa uchumi wamefafanua kuwa uwekezaji wa hekta 3.67 katikati ya jiji unajumuisha gharama kubwa za miundombinu ya kisasa, vikiwemo vyumba 93 vya biashara na kumbi za kimataifa, ambavyo thamani yake ni zaidi ya matofali yanayoonekana kwa macho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, amewataka wakazi wa Nyanda za Juu Kusini kutambua nafasi ya mkoa huo kama lango la SADC. Amesisitiza kuwa miradi kama City Park Garden inasaidia kuzuia fedha za kigeni zinazopotea nje, huku akikaribisha wananchi wote kuhudhuria Semina ya Uwekezaji Februari 17, 2026, ili kupata elimu rasmi badala ya kufuata maneno ya mitaani.
Huu ni wakati wa Watanzania kumiliki uchumi wao. TISEZA imeweka wazi kuwa milango iko wazi kwa kila mwenye nia ya kukuza kipato chake na Taifa kwa ujumla, ikiamini kuwa uwekezaji wa ndani ndio uti wa mgongo wa maendeleo endelevu.

0 Maoni